Chama cha ACT-Wazalendo leo Agosti 31, 2020 kimezindua Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu 2020 ikiwa na vipaumbele 10 vyenye majibu ya changamoto mbalimbali za Watanzania.
Chama hicho kimezindua ilani hiyo itakayowawezesha wagombea urais, ubunge na udiwani kuinadi katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Mbali na uzinduzi huo, pia Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe alimkabidhi Ilani hiyo, mgombea urais wa chama hicho, Bernard Membe na mgombea mwenza Omar Fakih Hamad ili waitumie kusaka kura kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Ilani hiyo, chama hicho kimejinasibu kutekeleza na kuvisimamia vipaumbele hivyo ambavyo ni pamoja na:- Ujenzi wa Demokrasia na utoaji Haki za watu, Ufanisi na ubora wa Huduma za jamii, -Uchumi wa watu, Uhuru kwa kila mtu na Elimu bora itakayotolewa bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu.
Vipaumbele vingine ni Kilimo cha kimapinduzi na mazingira wezeshi ya biashara, Usawa na Ustawi wa Wanawake na Vijana, Hifadhi ya Jamii kwa kila mtu/Afya bora kwa wote, Ushirika wa kisasa kwa maendeleo jumuishi, Haki za watu wenye ulemavu, Maji safi, Salama na gharama nafuu na ajira mpya milioni 10.
Aidha, akifafanua namna ahadi hizo zitakavyotekelezwa, Membe alisema kwa mara ya kwanza kati ya vya vyote vya siasa nchini, ilani hiyo imeainisha kila kipaumbele namna kitakavyotekelezwa.
Alitolea mfano Elimu ya Juu ambayo alisema atafuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuanza kutekeleza mfumo mpya wa kugharamia elimu hiyo.
“Serikali italipia Ada ya Masomo (Tuition Fee), Fedha za Vitabu (Stationeries), na gharama za Mafunzo kwa Vitendo (Field Studies/Internship) kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye Chuo Kikuu. Wanafunzi watachukua mikopo, Kwa wanaotaka, Kwa ajili ya gharama za maisha tu ( Meals and Accommodation ). Mfumo mpya utaanza Mwaka wa Masomo 2021/2022.
“Fedha za kutekeleza Elimu ya Ufundi na Elimu ya Juu zitatokana na mapato ya tozo ya kuongeza ujuzi (Skills Development Levy – SDL ). Tozo hii itatozwa kutoka Waajiri wa sekta binafsi na sekta ya Umma Kwa kiwango cha asilimia 2% ya gharama za mishahara,” alisema.
Katika hatua nyingine Membe alisema mazungumzo kuhusu ushirikiano wa Chadema na ACT Wazalendo kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu, yanaendelea hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.
“Kamati za pande zote mbili zinaendelea na mazungumzo kuhusu ushirikiano na sio muungano kwa sababu muungano unatakiwa kuwa kisheria na sasa muda wa kufuata sheria umekwishapita hivyo sasa tutashirikiana nje ya mfumo huo wa kisheria,” alisema.
Aidha, Zitto alisema kuwa kama ACT-Wazalendo kitashinda Uchaguzi Mkuu Serikali yake itasimamia uhuru, haki na Demokrasia kwa kufuta sheria kandamizi pamoja na kuanzisha timu ya majaji kwa ajili ya kuchunguza matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Ilani tunayoizindua leo imekidhi matakwa ya watanzania, imegusa Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa, na kijamii kwa ujumla ili kuweza kuwafanya watanzania waweze kufurahia rasilimali zao na kuwafanya waweze kufanya kazi na Bata” alisema.