Vitu vingine vilivyotolewa vilivyokuwa vimeziba njia ya haja kubwa na kumfanya apate maumivu makali ya tumbo ni vibiriti viwili vya gesi, mswaki na ganda la limao.
Dk Eliud Nyonyi aliyeshiriki kumfanyia upasuaji mgonjwa huyo amesema baada ya vitu hivyo kutolewa hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri.
“Hiyo picha inayosambaa mitandaoni sijaiona, lakini ni kweli kuna mgonjwa tumemfanyia upasuaji na tumemkuta hivyo vitu tumboni, ila siwezi kuzungumzia zaidi taarifa za mgonjwa,” alisema.
Picha inayoonyesha vitu hivyo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao mbalimbali huku kila mtu akisema lake kuhusu vitu hivyo.
Dk Nyonyi ambaye anakaimu nafasi ya mganga mkuu wa hospitali hiyo alimtaja mgonjwa huyo kuwa ni Eliud Novart (25) na kwamba, bado amelazwa katika wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji akiendelea kupatiwa matibabu.
Mganga mkuu wa wilaya
Akizungumzia tukio hilo, mganga mkuu wa Wilaya ya Missenye, Dk Hamis Abdallah alisema Novart alifikishwa katika Hospitali ya Mugana baada ya kupatiwa rufaa na Hospitali ya Nyakahanga iliyopo wilayani Karagwe akitokea Kyerwa.
Hata hivyo, Dk Abdallah alisema mgonjwa huyo alipofanyiwa kipimo cha x-ray alionekana kuwa na vitu ndani ya tumbo, ndipo Agosti 28 madaktari walipoamua kumfanyia upasuaji.
“Huyu mgonjwa baada ya upasuaji alikutwa na kijiko, vibiriti vya gesi, betri ndogo na ganda la limao na matibabu yake ni changamoto kwa kuwa mtu mwenyewe ni mgonjwa wa akili, kuna wakati anagoma kunywa dawa au kuchomwa sindano,” alisema Dk Abdallah na kuongeza kuwa kama angecheleweshwa kufikishwa hospitali kulikuwa na hatari ya utumbo kupasuka.
Alisema kwa mwonekano, vitu hivyo vinakadiriwa kukaa tumboni kwa takriban saa 48.
Mganga huyo wa wilaya alishauri wagonjwa wenye matatizo ya akili kupatiwa uangalizi wa kutosha na wasitengwe.
Aliwashauri ndugu kutokaa nao nyumbani, bali wawapeleke hospitalini ambako kuna kitengo cha kutoa ushauri kwa wagonjwa wa aina hiyo.
Daktari bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bohari alisema matatizo ya aina hiyo mara nyingi huwakumba watoto.
Alisema mara kadhaa watoto hupelekwa hospitali wakiwa wamemeza misumari au sumaku.
“Lakini kama ni msumari umekaa kwa urefu unaweza ukatoka kwa njia ya haja kubwa, lakini kama umekaa kwa mapana ni lazima upasuaji ili usije ukatoboa utumbo,” alisema.
Dk Bohari alisema yapo matukio pia ya wagonjwa kukutwa na nywele au kucha tumboni. “Kesi kama hizi hazielezeki, wapo wanaokula kucha na ukipiga x-ray unakuta tumboni fungu la kucha au nywele.”
Mtandao wa Rankers wa Uingereza umewahi kuripoti juu ya watu waliowahi kula vitu vya ajabu na mmojawapo ni Margaret Daalman wa Uholanzi aliyekutwa na seti nzima ya vijiko tumboni. Madaktari walivibaini vijiko hivyo baada ya kufikishwa hospitali akisumbuliwa na matatizo yanayoambatana na ujauzito na pia kuwa na hamu ya kula vitu vya chuma, tatizo ambalo kitaalamu huitwa Pica.
Mwaka 2010 mwanamume mwenye umri wa miaka 76 alikwenda hospitali, India akilalamika kuharisha na kupungua uzito na uchunguzi wa madaktari ulibaini tumboni mwake kuna kalamu ya wino ikilezwa kuwa alikuwa akijaribu kujikuna nayo kooni ikatumbukia. Mwaka 2009 mtoto Haley Lents wa Indiana, Marekani alikutwa na sumaku 10 zenye umbo la mviringo tumboni. Madaktari walisema alizimeza kwa kufananisha na peremende.
Tukio lingine ni la mwaka 2008. msichana mwenye umri wa miaka 18 wa India alipelekwa hospitali akilalamikia maumivu ya tumbo na kutapika, madaktari walimtibu sonona wakidhani anasumbuliwa na msongo wa mawazo kabla ya kubaini kuwa alikuwa na nywele zenye uzito wa kilo tatu tumboni.