Aliyetoka kwa Msamaha wa Rais, Anaswa Wizi wa Ng’ombe




JESHI la polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora kwa kushirikiana na wananchi, wamemkamata Hamisi Juma (29) anayedaiwa kuwa mwizi sugu wa ng’ombe ambaye pia aliachiwa kwa msamaha wa Rais John Magufuli.


 


Hamisi Juma alikamatwa mwishoni mwa wiki baada ya kukamatwa na ng’ombe 18 kati ya 25 walioibwa kwa mfugaji Madulu Shija (48) mkazi wa Kijiji cha Imalilo kata ya Ngulu.


 


Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Kamishna msaidizi Barnabas Mwakalukwa, amethibitisha kukamatwa kwa kijana huyo ambaye aliwahi kufungwa mara tatu gerezani kwa wizi wa mifugo.


 


Mwakalukwa alisema kijana huyo ambaye anaendelea kushikiliwa na Jeshi la polisi wilaya ya Igunga, alifanya tukio hilo Julai 28/2020 muda wa saa 5 usiku katika kijiji cha Imalilo kata ya Ngulu.


 


Alibainisha kuwa kijana huyo baada ya kufanikiwa kuiba ng’ombe hao 25 kwa Madulu Shija, aliondoka nao hadi kijiji cha Isugilo kata ya Igunga ambako aliomba kwa mama mmoja ambaye ni mfugaji awahifadhi ng’ombe hao.


 


Mwakalukwa alisema mama huyo alikubali kumsaidia kijana huyo hata hivyo, alimwambia akaripoti katika uongozi wa kijiji ambapo kijana huyo alipiga chenga hadi siku ya tatu alipoamua kuuza ng’ombe watatu kwa thamani ya Sh. 600,000.


 


Aidha, Mwakalukwa aliongeza kuwa baada ya mlalamikaji kutoa taarifa, polisi waliweka mtego katika minada yote ya Igunga ambapo Agosti 9 mwaka huu, walikamata ng’ombe watatu wakiuzwa katika mnada wa Igunga na walipowahoji wafanyabiashara waliokuwa na ng’ombe hao, ndipo walionyesha waliponunulia.


 


Alisema askari walikwenda hadi Kijiji cha Isugilo ambako walikamata ng’ombe 15 na kufanya hesabu kufi kia ng’ombe 18 huku ng’ombe saba wakikosekana.


 


Aidha, mtuhumiwa Hamisi Juma, naye alikamatwa siku hiyohiyo katika kata ya Iborogelo akinywa bia kwenye baa moja.


 


Kufuatia hali hiyo, kamanda Mwakalukwa alitoa onyo kwa wale wote ambao wanaendelea na uhalifu ikiwemo wizi wa mifugo na kusema kuwa wanapaswa kujitathimini kwa kuwa kazi ya wizi haina baraka kwa Mungu wala kwa jamii, hivyo wanatakiwa kuacha mara moja.


 


Mwakalukwa aliwataka wafanyabiashara wote wa mifugo mkoani Tabora kuacha utaratibu wa kununua ng’ombe wa wizi na badala yake wanunue ng’ombe halali, kwani jeshi la polisi litaendelea kufanya msako maeneo yote kwa wale wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi wa mifugo watachukulia hatua kali za kisheria.


 


Sanjari na hayo, kamanda huyo alisema baada ya mahojiano na kijana huyo, inaonyesha alishafungwa mara tatu kwa makosa ya wizi wa mifugo na baadaye kuachiwa mwaka jana kwa msamaha wa Rais.


 


Aidha, baadhi ya wananchi akiwemo mhanga aliyeibiwa, Madulu Shija, Lucia John, Jiganga Ngulunda na Rehema Mwandu, walilipongeza Jeshi la polisi Igunga kwa kufuatilia kwa karibu hadi kupata ng’ombe hao, huku wakidai kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad