Mgombea wa urais nchini Marekani kupitia chama cha Democratic Joe Biden anasema atafanya lolote lile linalohitajika ili kuiweka Marekani salama kutokana na janga la virusi vya corona hata ikiwa atalazimika kuufunga kabisa uchumi wa nchi hiyo.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini humo, Biden amesema atawasikiliza wanasayansi na kuchukua hatua watakazoshauri hadi pale virusi hivyo vitakapodhibitiwa.
Kinyume na anayoyasema Biden, Rais Donald Trump anatoa wito wa kufunguliwa kwa shule na watu warudi makazini.
Marekani imeandikisha zaidi ya visa milioni tano nukta tano vya maambukizi ya virusi vya corona huku idadi ya vifo ikipindukia 175,000.
Haya yanajiri wakati ambapo mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO akisema kuwa anatarajia janga la virusi vya corona litokomee katika kipindi cha miaka miwili ijayo.