WIKI hii imemalizika kwa tukio kubwa la Chama Cha Mapinduzi (CCM), kufanya mchujo wa mwisho wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, mchakato ambao umeshuhudia ukiwaacha nje baadhi ya wagombea walioongoza, wanasiasa wakongwe na wale waliokuwa wakisuburi huruma ya mwisho ya vikao hivyo vya juu.
Mchakato huo umefanyika, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu kundi kubwa, wakiwamo vijana, wanawake lionekane kujitokeza kuchanga karata za kuwania nafasi za ubunge na udiwani kupitia CCM.
Hamasa iliyoonekana CCM wakati wa mchakato wa ndani wa kutafuta wagombea kwa mwaka huu ilikuwa ni tofauti na miaka mitano, kumi, hata 15 nyuma, hata hivyo matokeo ya kura zilizopigwa na wajumbe wa chama hicho yalizua malalamiko mengi yakiwemo yale ya rushwa.
Hata hivyo suala la rushwa halijatajwa kama sababu ya moja kwa moja ya kuwaondoa baadhi ya wagombea ubunge na udiwani walioshinda kura za maoni.
Rais Dk. John Magufuli amekaririwa akisema kuwa iliwalizimu kutumia taarifa nyingi kuwajadili kwa muda mrefu ili wale watakaopitishwa wawe wenye uwezo.
Zaidi alisisitiza kuwa alipitia majina ya wagombea wote 10,367 waliochukua fomu na walioteuliwa ni wale wenye uwezo wa kuongoza, wazalendo, wenye kujitoa kwenye chama hicho, wanaofahamu mahitaji ya wananchi, wenye utayari wa kuwatumikia wananchi na wenye kukubalika kwa wananchi.
Rais Magufuli ambaye alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kilichokuwa na jukumu la kufanya uteuzi za mwisho wa majina ya wagombea wa nafasi ya ubunge katika majimbo mbalimbali alisema katika vikao walivyokaa kwa siku mbili (Agosti 18 na 19) walijadili majina ya wagombea kwenye ngazi ya Kamati ya Usalama na Maadili na kisha Kamati Kuu kwa uchambuzi wa kina.
Kwa maneno yake mwenyewe alisema; “Napenda niwahakikishie uchambuzi wa kina ulifanyika kwelikweli, tulitumia taarifa nyingi ambazo tulizipata kutoka katika vyanzo mbalimbali. Na mimi nataka kuwathibitishia wajumbe nimesoma majina yote 1,0367.
“Na hapa nina mabegi, mengine tunayo huko nyuma (huku akionyesha nyuma alipokuwa amekaa), hebu yainue hayo mabegi pamoja na lingine lipo pale, kwa yule atakayetaka ufafanuzi, kwa mtu yeyote ambaye anataka apewe ufafanuzi wa kina atapewa,” alisema Rais Magufuli.
Kabla ya uamuzi huu wa CCM, huko nyuma tuliisikia Takukuru ikieleza kuwa suala la malalamiko ya rushwa dhidi ya baadhi ya wagombea wa CCM wanakiachia chama hicho kwa sababu nao wana utaratibu wao wa kushughulikia mambo hayo.
Sisi tunaona kauli hii haiko sawasawa na inaweza kuja kutumika kama kielelezo huko mbele ya safari dhidi ya Takukuru.
Kwa sababu hiyo na ikizingatiwa sisi kama chombo cha habari kilicho na jukumu pamoja na mengine kuonya tulilisema jambo hilo mapema wakati wa mchakato wa wagombea kuchukua fomu na kuzirudisha kabla ya wagombea wenyewe kulalamika waziwazi wengine kwenye vyombo vya habari baada ya kura za maoni.
Sisi tunasema CCM imetekeleza wajibu wake, hata kama suala la rushwa halijatajwa moja kwa moja katika maamuzi iliyochukua, lakini Takukuru bado wanatakiwa kuja na jibu ya kuridhisha kwa Watanzania ambao kodi zao zinatumika kuendesha shughuli za taasisi mbalimbali za serikali ikiwamo kulipa mishahara.