CHADEMA Yaahirisha Zoezi la Mgombea wao Kuendelea Kutafuta Wadhamini Mikoani
0
August 21, 2020
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimelazimika kuahirisha zoezi la mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama hicho Mh,Tundu Lisu,kuendelea kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo taratibu za kujaza fomu kwa usahihi.
Uamuzi huo umetangazwa na mgombea wa Urais Tundu Lisu wakati wa ziara yake ya mwisho hii leo mjini Njombe huku akiomba radhi kwa wananchi wa mikoa iliyokuwa imesalia.
“Ratiba yetu ya mwanzo ilikuwa inasema baada ya mkoa wa Njombe, tungeenda Songea,Mtwara,Lindi halafu siku ya tarehe 21 Tungerudi Dar Es Salaam ili tarehe 22 twende Dodoma kuwasilisha fomu za uteuzi wa Rais na Makamu wa Rais”alisema Lisu
“Haitawezekana tena kwenda hiyo mikoa mitatu kwasababu ambazo zipo juu ya uwezo wetu,hizi fomu ni nyingi zinatakiwa kujazwa kwa usahihi,mikoa yote ambayo tumepita kazi mmefanya vizuri sana na kuna kazi ambayo katibu mkuu wetu anatakiwa aifanye kwa usahihi na kazi hiyo isipofanyika kwa usahihi katika sehemu zote nilizozisema hatuna mgombea na kama hatuna mgombea hatutakuwa na kampeni”aliongeza Lisu
Kwa upande wake mgombea wa Ubunge wa jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi (SUGU) aliyeongozana na viongozi wa kitaifa mkoani Njombe amewaomba wananchi wa jimbo la Njombe kuungana kwa sasa ili kufanikisha ushindi wa Chama hicho na kupata majimbo mengi.
“Nipo Njombe kwasababi ni kanda ya Nyasa na sisi kanda ya nyasa tunataka tuhakikishe tunakuwa na majimbo mengi zaidi na kura nyingi kwa ajili ya Urais ili kuing’oa serikali ya Chama cha Mapinduzi”alisema Sugu
Naye mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe Rose Mayemba kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Njombe amemshukuru kiongozi huyo kwa kufika mkoani Njombe kwani wamefurahishwa na ujio wake.
Tags