CHADEMA yaonya wagombea watakaosaliti chama



Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kanda ya Victoria inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, Zacharia Obad ametoa onyo kwa wanachama wa chama hicho waliopitishwa kugombea nafasi mbalimbali kutoleta visingizio ili wajitoe kushiriki uchaguzi Mkuu kwani kufanya hivyo ni usaliti kwa Chama. 


Alitoa onyo hilo wakati akizungumuza na wanachama waliopitishwa kuwania nafasi za udiwani na ubunge mkoani Mwanza ambapo alisisitiza hawategemei kuona hujuma ya aina yeyote kutoka kwa watu walioaminiwa na chama hicho, kwani chama kimefanya uwekezaji mkubwa kuanzia mchakato wa kura za maoni mpaka kuelekea kampeni zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu. 


Obad alisema iwapo mgombea ameshapitishwa  na wajumbe pamoja na kamati kuu ya chama, na yeye mwenyewe kwa hiari yake akakubali kuchukua fomu basi suala la kurejesha fomu na kushiriki uchaguzi mkuu ni lazima na siyo hiari tena vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaofanya hujuma ikiwemo kutorejesha fomu. 


Alisema haiwezekani mgombea apitie michakato yote kuanzia kutia nia, kupokea barua ya uteuzi, kuchukua fomu ya kugombea, kutafuta wadhamini na baadaye fomu yake kusainiwa na katibu wa chama kanda harafu baadaye kwa sababu zake tu binafsi asirejeshe fomu na ajitoe kushiriki uchaguzi kwa kuwa huo ni usaliti mkubwa. 


Aliongeza, inawezekana katika kipindi hiki baadhi ya wagombea wa Chadema wakafuatwa na vyama vingine na kushawishiwa kujitoa, mchezo ambao haukubaliki na chama na wote wenye mlengo huo ni lazima watambue habari za kukichezea chama zimeshafikia kikomo na hawatavumiliwa tena. 


Aidha, obad aliliomba jeshi la polisi kuhakikisha linatoa ushirikiano na ulinzi kwa wagombea wote katika kipindi cha kampeni bila kujali itikadi ya vyama vyao kwa kufanya hivyo itasaidia kulinda amani ya nchi ambayo ndiyo faraja ya kila mtanzania mwenye nia njema na taifa lake.


Pia alitoa shukrani za chama kwa mahakama zote nchini kwa kuwapa ushirikiano wagombea wote waliohitaji kusainiwa fomu zao ikiwemo wale wa Chadema ambapo aliiomba mahakama kuendelea kutimiza wajibu wake pasipo kuyumbishwa na mtu yeyote kwani watanzania wana imani kubwa na mahakama kama eneo sahihi la upatikanaji wa haki.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad