SERIKALI imesema inaweka mfumo imara wa kudhibiti wachezaji wa soka wanaosajiliwa nchini wawe na viwango vinavyotakiwa pamoja na vigezo vya kucheza kimataifa sambamba na kuchunguza rekodi zao huko walikotoka kabla ya kupewa leseni na kuanza kucheza ili kuondoa mambo ya ujanja ujanja yanayojitokeza hivi sasa na kuvuruga maendeleo ya soka nchini.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Agosti 11, 2020, na Dkt. Hassan Abbas, Msemaji Mkuu wa Serikali wakati akifanyiwa mahojiano na front Page ya +255 Global Radio.
“Wajibu wa Baraza la Michezo la Taifa unapaswa kuwa mkubwa kuliko sasa, tunaweka mifumo thabiti ya kuondoa ujanja ujanja kwenye sajili za wachezaji wa nje, kujiridhisha kuhusu rekodi zao, kwa maana unaweza kusajili mchezaji kumbe ni mwizi wa magari nyie mnashangilia tu, soon taratibu zitawekwa, hatuwezi kupokea pokea tu.
“Tunaandaa taratibu mpya, nakala za mikataba ya wachezaji zitapelekwa BMT kwa sababu wao wapo katikati ya Serikali na wadau, mtu akifoji mkataba, BMT watatusaidia kuweka bayana upi ni mkataba halali, haya mambo tunataka tuyakomeshe. Hili la Morrison acha lipite.
“Kuhusu mpango endelevu wa kuinua vipaji vya michezo kuanzia chini, hivi karibuni Serikali inakuja na mkakati wa kitaifa wa michezo ambao utawekeza sana katika kuandaa vipaji kuanzia chini, wapo wadau waosajili academy za mpira, TFF wamepata pesa za FIFA watajenga academy Tanga na Kigamboni, serikali itaandaa Chuo cha Malya kwa ajili ya Sports Officers, mpira utafundishwa kisayansi.
“Pale wizarani tuna mainjinia wataalama wa michezo, wamesoma vizuri China na nchi nyingine, wakati wamekuja Everton wataalam wetu wamefundishwa namna ya kutibu nyasi, unajua nyasi zinaumwa, hawa wanatusaidia mdau akitaka kujenga uwanja wanamshauri.
“COSOTA imesharudi nyumbani, sisi kazi yetu ni kuhakikisha changamoto zilizokuwepo tunazishughulikia, tumeshaanza kukusanya kila kilichokuwepo kwenye akaunti ya COSOTA, kila msanii na wadau wote wenye haki zao watazipata, tutatangaza,” Dkt. Abbas.