SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) ni kama limemaliza utata wa usajili wa mchezaji Bernard Morrison aliyetua Simba huku akiwa na mvutano na klabu yake ya zamani ya Yanga, baada ya mtandao wao wa usajili kuonyesha kuwa ni mali ya Simba.
Usajili wa Morrison kutua Simba ulivuta hisia za mashabiki wa pande zote mbili za Simba na Yanga kufuatia suala la kimkataba lililokuwa likimkabili hadi pale maamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kutoa maamuzi ya mchezaji huyo kuwa huru, hivyo kuangukia Simba.
Akizungumza na Championi Ijumaa, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amesema kuwa, hadi sasa bado anashangazwa na uongozi wa Yanga kuendelea kulalamika juu ya usajili wa Morrison huku mtandao wa Fifa ukiweka wazi kuwa mchezaji huyo ni mali ya Simba.
Aidha, aliongeza kuwa iwapo Yanga watahitaji kesi ya Morrison kusikilizwa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), watatakiwa kutoa euro 15,000 ambazo ni zaidi ya Sh 40m ndipo suala lao lisikilizwe ikiwa ni kwa jaji mmoja na wakihitaji zaidi itabidi waongeze fedha.
“Suala hili linachekesha kwa sababu, sidhani kama viongozi wa Yanga hawajui sheria, wanaijua vizuri, Morrison alikuwa mchezaji huru, kwenye mtandao wa Fifa inaonyesha amesajiliwa Simba, mtandao huo unajieleza kabisa kuwa msimu wa 2019/20 alikuwa mchezaji wa Yanga na msimu ujao wa 2020/21 ni mchezaji wa Simba. Hii inaonyesha katika sehemu ya uhamisho wa mchezaji.
“Sijajua Yanga hadi leo wanacholalamika ni nini kuhusiana na mchezaji huyo, mwenyekiti wa kamati ya hadhi za wachezaji alitamka hadharani kuwa mkataba ule una upungufu, lakini hata wakienda CAS wanaweza wasifanikishe, kwanza siyo kazi nyepesi hadi kufikia kesi kusikilizwa, inaweza kuchukua muda mrefu hata mwaka mmoja kama ilivyokuwa kwa Okwi wakati tunawadai Etoile Du Sahel.
“Unatakiwa kuwakilisha dokumenti zote Fifa kisha wao ndio wakupangie jaji ambaye atatakiwa kulipwa euro 15,000 kwa jaji mmoja ambapo pia itategemea kesi inahusu nini na iwapo atatakiwa kuongezwa jaji wa pili ili aweze kusikiliza basi pesa zinaongezeka, hivyo ni vyema waweke risiti hadharani, isije wakatumia muda huu kuwahadaa mashabiki wao,” alisema Rage.