MFANYAKAZI za ndani ‘Hausigeli’ aliyefahamika kwa jina la Zaina Ismail, ametiwa mbaroni na jeshi la polisi, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam kwa mauaji ya mtoto wa bosi wake.
Zaina ambaye ni mkazi wa Yombo Buza, Dar anatuhumiwa kumuua mtoto aitwaye Abraham Thomson mwenye umri wa mwaka mmoja.
Akizungumzia tukio hilo babu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Daud mkazi wa Kiwalani amesema tukio hilo limetokea Julai 20, mwaka huu.
Inaelezwa kuwa, siku ya tukio hilo mama wa marehemu aitwaye Anslata Chitanda ambaye ni mke wa mwanaye Fredrick Daud wakazi wa Yombo Buza, alimuachia mwanaye Hausigeli huyo naye kwenda hospitali.
“Baada ya muda huyo Hausigeli alimpigia simu mama wa mtoto na kumuambia arudi haraka nyumbani kwani alimuona mtoto kama amepata tatizo.
“Baada ya taarifa hiyo mama yake alirudi na kumkuta mwanaye amelala kitandani, lakini tayari alikuwa ameshafariki.
“Ikabidi wanipigie simu ambapo mimi pia nilikwenda mpaka huko walipokuwa wakiishi.
“Nilipoingia ndani nikakuta kweli mjukuu wangu ameshafariki dunia.
“Tukakubaliana msiba tuuleta hapa ninapoishi na mwili wa marehemu tukaenda kuuhifadhi Hospitali ya Temeke.
“Lakini kutokana na kifo cha utata cha mjukuu wangu ikabidi ndugu wengine wampane huyo mfanyakazi wa ndani.
“Mara huyo binti akaanza kulia na kukiri kwamba yeye ndiyo amehusika na mauaji ya huyo mtoto,” alisema babu wa marehemu Abraham
Aliongeza kuwa, walipoendelea kumhoji binti huyo alimfanyaje mtoto mpaka akafariki dunia alisema, alitumia mbinu za kishirikina.
Hata hivyo, kwa kuwa Amani Mtandaoni siyo muumini wa imani za kishirikina maelezo mengine ya huyo binti yanawekwa kapuni.
Aidha, babu wa marehemu aliendelea kumweleza mwandishi wetu kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kukiri, aliiomba familia imsamehe kwa sababu wakati akimfanyia marehemu vitendo hivyo vya kishikina hakuwa amekusudia kumuua.
Babu huyo wa marehemu Abraham anasema: “Hivyo ikabidi huyo Hausigeli tumpeleke Kituo cha Polisi cha Yombo Makangarawe ambapo walituambia kwa suala hilo tumpelekea Kituo cha Chang’ombe, wilayani Temeke ambapo ndipo wangeweza kuimudu kesi hiyo, na kweli tulifanya hivyo.”
Inaelezwa kuwa, baada ya polisi kumshikilia mtuhumiwa kwa uchunguzi familia iliambiwa iupeleke mwili wa marehemu Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi wa chanzo cha kifo.
Wakiwa huko babu huyo amesema, mwili ulifanyiwa uchunguzi na ripoti ya kitabibu kuonesha kuwa marehemu alikufa kwa kukosa hewa.
“Tumeambiwa sehemu zote hazikuwa na tatizo isipokuwa imebainika kuwa alikosa pumzi,” alimaliza kusema.
Baada ya kumsikiliza Babu wa marehemu mwandishi wetu alizungumza na mama wa marehemu (Anslata) ambaye alisema hatokisahau kifo cha mwanaye ambacho kimegubikwa na utata mkubwa.
“Yule Hausigeli alikuwa na mapenzi makubwa sana na mwanangu lakini hiki kilichotokea kinanishangaza sana.
“Mwanangu hakuwa na raha bila kumuona huyo dada wa kazi, ndiyo maana nilimuamini kiasi cha kumuachia mwanangu.
“Sasa siku ya tukio nikiwa hospitali alinipigia simu nirudi nyumbani, mtoto alikuwa amepata tatizo, nilipofika nikamkuta amelazwa kitandani nilipomtazama vizuri alikuwa ameshakufa.
“Tulivyombana sana dada wa kazi akaanza kusema anahusika na kifo cha mwanangu kwa njia za kishirikina.
“Yaani roho inaniuma sana nikimkumbuka mwanangu ambaye hivi juzi juzi ndiyo tulimfanyia bethdei ya kutimiza mwaka mmoja lakini yote hayo namuachia Mungu,” alimaliza kusema mama huyo na kuomba aachwe apumzike kwani asingeweza kuongea kutokana na uchungu alionao.
Tukio hili ni la pili ndani ya mwezi huu kwa watumishi wa ndani kuua watoto wa bosi zao ambapo hivi karibuni shambaboi, Yasin Abdallah (35) mkazi wa Kijiji cha Kwazoka, Kata ya Vigwaza mkoani Pwani aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kuua watoto wawili wa bosi wake kwa kuwacharanga mapanga.
Mbali na kufanya tukio hilo la kinyama, mfanyakazi huyo wa ndani wa kiume alimjerhusi pia mke wa bosi wake aitwaye Saada Maulidi kwa kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali mwilini.
Matukio haya ya kikatili yanayofanywa na watumishi wa ndani yameshtua wengi na hivyo tahadhari kutolewa kwa wazazi kuwa makini na hausigeli, hausiboi katika kuishi nao.
“Jamani wazazi tuwe makini, hawa watumishi wa ndani ni watu hatari sana, watatumaliza,” aliandika mama mmoja kwenye ukurasa wa Instagram uliyoposti tukio la Saada kujeruhiwa na shambaboi wake.
Watoto wa Saada, Rehema Azizi (5) na Abubakari Azizi (7) waliuawa kinyama na shambaboi huyo muda mfupi baada ya kutoka shambani huku sababu ya kufanya hivyo ikishindwa kujulikana.
Baba wa watoto hao wawili ambao ni marehemu, Azizi Makoloka alisema, alikuwa anaishi na Yasin vizuri na kushangazwa na roho iliyomuingia Julai 8, mwaka huu hadi kufikia hatua ya kuwaua wanaye na kumjeruhi vibaya mkewe kwa mapanga.