Baadhi ya vyama vya siasa nchini tayari vimekwishateua Wabunge watakaopeperusha bendera ya vyama vyao katika Uchaguzi Mkuu ujao, utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu, ikiwemo CHADEMA na ACT Wazalendo.
Bendera ya Chama cha ACT Wazalendo na CHADEMA
Kwa upande wa CHADEMA tayari kimekwishataja majina ya wagombea wake kwa awamu tatu tofauti, na kati ya hao walioteuliwa, ambao wamekwishachukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi hadi sasa ni Joseph Mbilinyi wa Jimbo la Mbeya Mjini, Peter Msigwa Jimbo la Iringa, Ester Bulaya Jimbo la Bunda Mjini, Halima Mdee Jimbo la Kawe, John Heche wa Jimbo la Tarime Vijijini.
Wengine ni Joseph Haule wa Jimbo la Mikumi, John Mrema Jimbo la Segerea, Devotha Minja Jimbo la Morogoro Mjini, Rhoda Kunchela Jimbo la Mpanda Mjini, Jesca Kishoa Jimbo la Iramba Magharibi, Boniface Jacob wa Jimbo la Ubungo, Jimbo la Vunjo ni Grace Kihwelu na Henry Kilewo wa Jimbo la Mwanga pamoja na Ezekia Wenje wa Jimbo la Rorya.
Kwa upande wa chama cha ACT Wazalendo, mpaka sasa waliochukua fomu hizo ni pamoja na Webiro Wakazi Wassira ambaye anagombea Jimbo la Ukonga, Mwanaisha Mndeme ambaye ni mgombea wa Jimbo la Kigamboni pamoja na Saed Kubenea ambaye anagombea Jimbo la Kinondoni.
Mpaka sasa Chama cha Mapinduzi, Chama cha CUF, CHAUMMA, SAU, CCK, ADC, UPDP, NRA, AAFP pamoja na DP, bado havijatangaza majina ya Wagombea wa nafasi ya Ubunge.