Jinsi ya Kurudisha Hamasa iliyopotea Katika Kazi
0
August 05, 2020
Wakati unapokutana na kitu kipya, au unapofanya jambo fulani kwa mara ya kwanza, ni lazima utajisikia mwenye hamasa kubwa.Lakini kama inavyosemekana kwamba;hakuna marefu yasiyokuwa na ncha. Ndivyo hivyo pia kwenye hamasa, kwani hali hii nayo huwa ina mwisho wake. Kuna wakati unaweza kujisikia mwenye hamasa na kwa wakati mwingine ukahisi kutokuhamasika.
Wengi huzianza shughuli zao kwa hali na kasi mpya, ila baada ya muda fulani zile nguvu zao huanza kufifia na kupotea kabisa. Kuwa na hamasa wakati wote kamwe haliwezi kuwa jambo rahisi. Ni jambo linalohitaji nidhamu na juhudi binafsi. Na katika makala yetu ya leo nakushirikisha baadhi ya zana muhimu unazoweza kuzitumia ili kuweza kupata na kurudisha hamasa yako. Karibu tujifunze kwa pamoja..
1. Tumia muda wako pamoja na watu wanaohamasika na kuhamasisha.
Kuna msemo wa kiingereza unaosema kwamba “birds of the same feathers flock togeher”, ukiwa na maana kuwa “ndege wenye mabawa ya kufanana huruka pamoja”.Ukweli ulio wazi ni kuwa namna tunavyofikiri na kutenda kunaathiriwa zaidi na mazingira yetu.
Ukitaka kuwa na fikra chanya jiweke kwenye mazingira chanya,na ukitaka kuwa na fikra hasi jiweke kwenye mazingira hasi.Na ndivyo hivyo pia kwenye hamasa, ili uweze kuwa mwenye hamasa basi shirikiana na aina ya watu wenye kuhamasika na kuhamasisha.Ni muhimu kuwa makini na aina ya watu unaotumia muda wako kushirikiana nao.
2. Ikumbuke shauku yako ya awali.
Kuna baadhi ya vitu fulani ambavyo hapo kabla ulikuwa ukivifanya mara kwa mara.Unachotakiwa kukifanya hapa ni kuikumbuka shauku yako ya awali.Kwa mfano; tuseme kwamba hapo kabla ulikuwa na mazoea ya kufanya meditation (tahajudi),kusoma sana vitabu, na kufanya mazoezi mara kwa mara.
Sasa basi ili uweze kuirudisha hamasa yako unapaswa kukumbuka kuhusiana na mambo hayo. Na unapokuwa ukifikiria kuhusiana na vitu hivyo,unapaswa pia kukumbuka namna ulivyokuwa ukijisikia kama matokeo ya kile ulichokuwa unakifanya. Na kwa kufanya hivyo kwa muda mrefu utaanza kujiskia vizuri,mchangamfu, na mwenye hamasa pia.Weka umakini wako katika kufikiria hilo kwa muda mrefu na utahisi mabadiliko.
3. Ishi maisha rahisi.
Katika maisha yetu ya sasa, tumekuwa wazuri sana katika kujiongezea matatizo yasiyo ya lazima.Tumekuwa tukijiingiza wenyewe katika vikwazo na vitu ambavyo vinaweza kuvutia mbali mawazo yetu (udaku,umbea,kulalamika,n.k).Na kadri tunavyozidi kukazia fikra zetu kwenye mambo hayo ndivyo inavyozidi kuwa ngumu kwetu kuhamasika.Ondokana kabisa na mambo ya aina hiyo.
4. Kuwa na vipaumbele.
Wakati mwingine hali ya kukosa hamasa huwa inasababishwa na wengi wetu kutokuwa na vipaumble. Tunashindwa kukazia fikra zetu kwenye kitu kimoja,na matokeo yake tunajikuta tukijaribu kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Ni ngumu sana kuwa na hamasa ikiwa fikra zako zipo kila mahali. Ni muhimu tukawa na vipaumbele,na tutumie muda wetu katika mambo yaliyo ya muhimu.Na kwa kuwa na vipaumbele itakufanya ujisikie vizuri,mwenye nguvu,na mwenye hamasa pia.
Hayo ni baadhi ya mambo machache unayoweza kuanza kuyatumia sasa ili kuweza kupata na kurudisha hamasa yako iliyopotea.Nakutakia kila la kheri na utekelezaji mwema kwa kile unachojifunza hapa.Endelea kutembelea mtandao huu kwa ajiri ya kujipatia mambo mengi mazuri ya kuelimisha na kuhamasisha pia. Washirikishe na wenzako pia ili nao waweze kujipatia mambo haya mazuri.
Na. Geofrey mwakatika.
Tags