Mbunge wa Ubungo aliyemaliza muda wake Saed Kubenea, amesema kuwa ameamua kuachana na Jimbo la Ubungo kwa kuwa endapo angegombea tena kulikuwa na hatari ya Jimbo hilo kuchukuliwa na CCM, na hivyo yeye hataki kushiriki dhambi hiyo ya kuisaidia CCM kupata Jimbo.
Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kuongeza kuwa hata kama angegombea angeshinda na kutoa ushauri kwa wagombea wa upinzani katika jimbo hilo kukaa chini na kukubaliana ili aweze kusimama mmoja ili kuepukana na athari ya kugawana kura.
"Niliona kwamba nikigombea Jimbo la Ubungo kuna uwezekano mkubwa wa sisi wagombea wa upinzani kugawana kura na jimbo hilo kwenda CCM, kama ilivyotokea 2015 katika Jimbo la Segerea, kwahiyo nikasema mimi sitaki kushiriki dhambi ya kusaidia jimbo hilo kwenda CCM na ndiyo maana nikaamua kuachana na Jimbo hilo kwa sababu kazi yangu nimeifanya", amesema Kubenea.
Awali Kubenea alikuwa ni Mbunge wa Ubungo kupitia CHADEMA, lakini kutokana na sababu zake alizozitaja aliamua kukihama chama hicho na kuhamia chama cha ACT Wazalendo na kutia nia Jimbo la Kinondoni.