Majimbo Matatu Pasua Kichwa Uchaguzi Mkuu 2020



DAR: WAKATI mchakato wa kuwapata wagombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukizidi kushika kasi, majimbo matatu ya Arusha Mjini, Mbeya Mjini na Tarime Vijijini, yameelezwa kuwa pasua kichwa kutokana na mchuano mkali unaotarajiwa kuelekea Oktoba 28, 2020. RISASI linachambua…………



Mchuano huo unatarajiwa kuhusisha CCM na Chama kikuu cha upinzani nchini- Chadema ambacho wagombea wake wanatetea majimbo hayo ilhali CCM ikijiapiza kurudisha himaya yake.



Majimbo hayo yamekuwa na mvuto wa kipekee baada ya wagombea waliojitokeza na kushinda katika mchakato wa kura za maoni CCM, kunogesha mpambano kutokana na mizizi waliyojijengea kisiasa huku umaarufu wa majina yao ukizidi kuwapasua kichwa wapiga kura.



ARUSHA MJINI

Mojawapo ya jimbo linalotazamiwa kunogesha uchaguzi mkuu ni Arusha Mjini ambalo mpambano wake unatarajiwa kuwa kati ya Mbunge aliyemaliza muda wake, Godbless Lema (Chadema) na Mrisho Gambo kutoka CCM.



Gambo ambaye alikuwa miongoni mwa makada 29 wa CCM waliokuwa wamechukua fomu kuwania jimbo hilo, aliibuka kidedea baada ya kupata kura 333 akifuatiwa na Philemon Mollel aliyepata kura 68 katika mchakato huo. Kutokana na matokeo hayo, Gambo anaweza kupata nafasi ya kuiwakilisha CCM katika jimbo hilo katika uchaguzi wa Oktoba 28, mwaka huu.



Ikiwa hali itakuwa hivyo, jimbo hilo litakuwa na ushindani wa kipekee hasa ikizingatiwa kuwa Gambo ambaye amekuwa mkuu wa mkoa huo kuanzia 2016 hadi Juni mwaka huu, amejijengea mizizi katika jimbo hilo, hali ambayo iliibua mivutano kati yake na watendaji wengine wa serikali.



Kinyang’anyiro ndani ya CCM ndicho kinachoelezwa kusababisha anguko lake katika nafasi ya mkuu wa mkoa. Kwa mantiki hiyo, iwapo akipitishwa, hawezi kupepesa macho katika kuhakikisha analinyakua mikononi mwa Lema.



Hata hivyo, Lema ambaye anatajwa kuwa mtoto wa mjini, hawezi kuliachia jinbo hilo kirahisi kutokana umahiri wake ambao amejijengea tangu mwaka 2010.



MBEYA MJINI

Katika jimbo la Mbeya Mjini, mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya Joseph Mbilinyi ‘Mr Two, Sugu’ (Chadema) na Dk. Tulia Ackson (CCM).



Licha ya kwamba CCM bado haijampitisha Dk. Tulia kuwania jimbo hilo, tayari naibu spika huyo amejiwekea mizizi katika jimbo hilo kwa muda mrefu ikiwamo kuanzisha taasisi ya Tulia Trust na mashindano mbalimbali ili kujiweka karibu na wapiga kura wa jimboni.



Aidha, Dk.Tulia pia alitoa zaidi ya Sh milioni Sh.820.39 kusaidia sekta za elimu, afya, maji, miundombinu, uwezeshaji mikopo kwa vikundi na utawala, jambo ambalo lilitafsiriwa kuwa ni kummaliza nguvu Sugu.



Tayari Dk. Tulia ameshavuka hatua ya kwanza baada ya kushinda katika kura za maoni ndani ya CCM, kwa kupata kura 843 katika ya kura 924 zilizopigwa.



Mshindi wa pili ni Dk. Mahande Mabula ambaye alipata kura 16 na wa tatu kura 11 ambaye alikuwa Charles Mwakipesile.



Hata hivyo, Sugu mara kwa mara amekuwa akijinasibu kumkabili mwanamama huyo kwa kile anachoamini kuwa bado anakubalika kwa wapiga kura wake ambao wamemwamini tangu 2010.



TARIME VIJIJINI

Katika jimbo hilo ambalo lilikuwa linashikiliwa na John Heche (Chadema), limeendelea kuwatoa jasho watia nia wa CCM baada ya kada mkongwe wa Chadema aliyehamia CCM mwaka jana na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri Tamisemi, Mwita Waitara kutangaza kukabiliana na Heche.



Waitara ambaye alikuwa Mbunge wa Ukonga (CCM), tayari ameibuka kidedea kwa kupata kura 291 katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.



James Bwire alipata kura 135 na kushika nafasi ya pili wakati nafasi ya tatu ikienda kwa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi mwenye kura 128.



Waitara ambaye alikuwa Mbunge wa Ukonga, Bunge lililopita alianza harakati mapema za kuwania jimbo hilo hadi akapatwa na msukosuko baada ya CCM mkoa wa Mara kumweka kitimoto kwa kile walichodai ni kuanza kampeni mapema.



Aidha, amekuwa akijinasibu kuwa, “Heche ni kinyago nilichokichonga, nikikutana naye Tarime nitamshikisha adabu.” Ilihali Heche ambaye ameshika jimbo hilo, anadaiwa kujijengea misingi ndani ya jimbo hilo.



Akizungumzia mchuano ndani ya majimbo hayo matatu, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk. George Kahangwa, alisema ushindani huo ni moja ya mambo ambayo Watanzania au wapiga kura, hupendelea kuona kipindi cha chaguzi.



“Kwa sababu jimbo likiwa na mgombea mmoja dhaifu, huku chama kingine kikiwa na mgombea mwenye nguvu zaidi, uchaguzi hukosa mvuto na hata ushiriki wa wapiga kura nao huwa mdogo, lakini sasa hali ikiwa hivyo kwenye majimbo hayo matatu, watu wengi watajitokeza kupiga kura kutokana na hamasa iliyopo, ni sawa na mechi za watani wa jadi,” alisema Dk. Kahangwa ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad