Mambo 10 ya kuzingatia kabla na wakati wa kuendesha gari umbali mrefu
0
August 28, 2020
Kuendesha gari ni suala linalohitaji umakini na utulivu mkubwa, hasa pale unapoendesha gari umbali mrefu. Mara kwa mara kumeshuhudiwa ajali mbalimbali ambazo kimsingi zinatokana na madereva kutokuzingatia kanuni muhimu katika utumiaji wa vyombo vya usafiri.
Ili kuhakikisha usalama wako pamoja na watumiaji wengine wa barabara, yapo mambo kadhaa unayopaswa kuyazingatia kabla na wakati wa kuendesha gari umbali mrefu.
1. Kagua na andaa gari
Kabla ya safari yoyote gari linahitaji kukaguliwa na kuandaliwa, hasa kabla ya safari ndefu. Kuna mambo kadhaa unayohitaji kuyakagua kwenye gari lako:
Kagua hali na ubora wa magurudumu. Hakikisha magurudumu yamejaa vizuri na hayajazeeka.
Kagua mafuta lainishi (oil). Hakikisha gari yako ina mafuta lainishi ya kutosha tena ya ubora unaotakiwa.
Kagua kiasi cha maji. Maji? Ndiyo maji ni muhimu sana kwenye gari kwa ajili ya kupooza injini ya gari pamoja na kusafishia vioo.
Kagua utendajikazi wa injini. Hakikisha injini yako inafanya kazi vizuri.
Kagua sehemu nyingine za gari kama vile breki, kiongeza mwendo (accelerator), usukani, taa, honi, viashiria (indicators), n.k.
Usibebe mizigo isiyokuwa ya lazima kwenye gari. Hii itakupotezea mafuta na nafasi bila sababu.
Hakikisha unalikagua gari lako vyema na kuliandaa kwa ajili ya safari. Unaweza pia kumtumia mtaalamu wa magari ili akusaidie kulikagua na kuliandaa kwa safari yako.
2. Pumzika
Ili uweze kuendesha gari vyema wakati wa safari ndefu ni muhimu kupumzika kwa kiasi cha kutosha kabla na wakati wa safari.
Hakikisha kabla ya safari unapata muda wa kutosha wa kulala ili kuepusha kusinzia barabarani kunakoweza kusababisha ajali. Unapokuwa barabarani unaweza pia kupumzika baada ya umbali fulani ili usichoke sana.
Kumbuka! Kupumzika uwapo safarini kutakuwezesha kupata nguvu zaidi na kutoa nafasi ya gari lako kupoa ili kuepusha ajali ya gari kuwaka moto.
3. Fahamu sheria na kanuni
Kuna kanuni zinazotawala matumizi ya barabara pamoja na vyombo vya usafiri. Ili kuepuka kuingia kwenye matatizo, hakikisha unafahamu vyema sheria za barabarani za eneo unalokwenda. Unaweza kuzingatia haya:
Beba vibali na nyaraka muhimu za dereva na gari Mf. leseni, bima, n.k.
Kama utavuka mipaka ya nchi beba pasi ya kusafiria pamoja na Visa kama inahitajika.
4. Beba vitu muhimu
Kama ilivyo ada, safari inahitaji maandalizi. Hakikisha unabeba vitu muhimu unavyoweza kuvitumia kwenye safari yako kama hivi vifuatavyo:
Chakula na vinywaji. Ikiwa hutonunua chakula au kupata mahali pa uhakika pa kununua chakula na vinywaji, basi beba chakula chako utakachokula mara uwapo safarini.
Beba kisanduku cha huduma ya kwanza. Ni muhimu kuwa na kisanduku cha huduma ya kwanza kwenye gari ili upatapo tatizo la kiafya kikusaidie.
Beba vifaa vya msingi vya matengenezo ya gari. Vifaa kama vile jeki, spana, tochi, n.k. ni muhimu sana.
5. Tumia mafuta vizuri
Hakikisha unatumia mafuta vizuri mara uendeshapo gari umbali mrefu ili kuhakikisha unapunguza gharama zisizokuwa za lazima.
Hakikisha pia huachi kiwango cha mafuta kipungue sana ili usije ukaishiwa mafuta kwenye eneo ambalo liko mbali na kituo cha mafuta.
6. Usitumie kilevi
Chanzo kikubwa cha ajali ni ulevi au matumizi ya pombe kwa madereva. Pombe hukufanya ushindwe kumudu gari vyema, hivyo usitumie kilevi kabla na wakati wa safari.
7. Fahamu kuhusu hali ya hewa
Safari yako inaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya hewa. Hivyo ni vyema ukahakikisha unafahamu hali ya hewa ya eneo unalokwenda ili ujiandae mapema.
Kwa mfano kama kunatarajiwa kunyesha mvua, ni vyema ukachunguza kama barabara utakayoitumia kama huwa inapitika wakati wa mvua ili usije ukakwama.
8. Endesha kwa mwendo wa wastani
Mwendokasi ni chanzo kikubwa cha ajali na matatizo mengi barabarani. Ni muhimu kuendesha gari kwa mwendo wa wastani ili kuepusha matatizo yasiyokuwa na ulazima.
Kumbuka! Unapoendesha gari kwa mwendo wa wastani ni rahisi kujihami mara kunapotokea tatizo barabarani.
9. Zingatia burudani
Burudani tena? Ndiyo, unaweza kubeba miziki ambayo itakuburudisha wewe pamoja na wale unaosafiri nao ili msichoke muwapo safarini. Kusikiliza mziki wakati wa kuendesha gari kutakuweka katika hali (mood) nzuri sana.
10. Fahamu vyema eneo unalokwenda
Je unafahamu vyema barabara utakayoitumia kufika kwenye eneo unalokwenda? Ili kuepuka kupotea au kukwama kwenye safari yako, ni muhimu ukafahamu vyema eneo unalokwenda.
Unaweza kuwauliza watu wanaofahamu eneo hilo au kutumia ramani mbalimbali kama vile Ramani za Google.
Pasipo shaka naamini umeona jinsi ambavyo kuendesha gari umbali mrefu kunavyohitaji maandalizi na mikakati muhimu. Kwa hakika ukizingatia mambo haya yaliyoelezwa hapa utaweza kuwa na safari salama yenye amani na furaha.
Tags