KAMATI ya Maadili, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mghana, Bernard Morrison.
Hiyo ikiwa ni siku moja imepita tangu Simba imtangaze kiungo huyo kupitia mitandao ya kijamii kwa kuachia picha zikimuonyesha amevalia jezi za timu hiyo huku akiwa anasaini mkataba.
Mghana huyo hivi karibuni aliitwa kuhojiwa na TFF kufuatia kudai kuwa hana mkataba na Yanga wakati Yanga wao wakidai wana mkataba naye wa miaka miwili ambao utamalizika Julai 2022.
Wakati kukiwa na sintofahamu hiyo, juzi Simba walimtambulisha kama mchezaji wao rasmi.
Katika maamuzi yatakayotolewa leo na TFF, huenda yakabariki kiungo huyo kwenda kuichezea Simba katika msimu ujao kutokana na mkataba wake na Yanga kuwa na upungufu kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Championi Jumatatu.
Yapo mambo manne yatakayobariki kiungo huyo mwenye mbwembwe nyingi uwanjani ikiwemo staili yake ya kuupanda mpira kwa juu wakati anaukokota, kwenda Simba. Lakini lolote linaweza kutokea ikiwemo Yanga kushinda, kwa kuwa nao waliwasilisha utetezi wao. Mambo hayo manne ni;
Tarehe ya mkataba wa mwanzoMkataba wa mwanzo wa miezi sita kati ya Yanga na Morrison, unaonyesha upungufu na kujichanganya kwa Yanga juu ya Morrison. Tarehe ya mkataba wa mwanzo wa miezi sita alioupelekwa TFF unaonyesha alisaini mkataba Desemba 17 alipotua nchini, wakati dirisha la usajili lilifungwa Desemba 15. Maana yake alisaini nje ya muda wa usajili, kwa hiyo ni kama mkataba huo haukuwa halali.
Mghana huyo yeye mwenyewe hivi karibuni alisisitiza kuwa alicheza michezo ya ligi ukiwemo ule wa kwanza alioucheza na Singida United bila ya kuwa na mkataba huku akisema saini iliyokuwepo katika mkataba uliowasilishwa na Yanga TFF, siyo yake.
Inaonekana alisaini mkataba wa awali tu YangaSiku zote mkataba wa awali (pre contract), haumzuii mchezaji kusaini mkataba kwenye klabu nyingine itakayomhitaji.
Championi Jumaatu, limenasa taarifa kuwa kiungo huyo alisaini mkataba wa awali kwamba wakipata fedha za usajili, atakuwa tayari kusaini miaka miwili Yanga kama wakitimiza makubaliano waliyokubaliana kwenye mkataba wa awali aliosaini. Lakini wakati akiwa amesaini mkataba wa awali, Simba wakamfuata na dau kubwa ndiyo akamwaga wino. Pre contract haina nguvu kisheria kumzuia mchezaji kusaini timu nyingine.
Mkataba wake una ukurasa mmoja uliotiwa sainiHofu kubwa ipo hapa, ni kutokana na mkataba ulioonyeshwa akiwa anasaini una ukurasa mmoja tu ambao una saini ya Morrison, wakati mikataba yote inatakiwa kuwa na kurasa nyingi ambazo zinachambua vizuri vipengele na masharti, na kila ukurasa unapaswa kuwa na saini ya mhusika ili kuepuka ujanja wa kuongeza ukurasa mwingine katikati usiotambulika. Hiyo inaonyesha kwamba mkataba huo hauwezi kuwa halali.
Mkataba hauna saini ya dole gumbaKati ya utata mkubwa uliojitokeza katika mkataba huo ulioonyeshwa na GSM ambao wenyewe unaonyesha saini ya kawaida, wakati mikataba yote ni lazima iwe na sehemu ya kusaini kwa dole gumba.
Hiyo ndiyo sababu ya Simba kuachia picha ya ikimuonyesha kiungo huyo anasaini mkataba huku akipiga saini ya dole gumba, ikimaanisha kuwa Yanga walikosea hapo katika kumsajili kiungo huyo.
WILBERT MOLANDI NA MARCO MZUMBE