Gari ni kifaa au chombo kinachorahisisha usafiri, lakini kinapaswa kutumiwa kwa tahadhari kubwa. Ajali zinazotokana na magari kuwaka moto, mara kadhaa zimekuwa zikisababisha hasara kubwa au hata kugharimu maisha ya watu.
Kwa hakika jambo hili si zuri, hivyo kila dereva au mtumiaji wa gari ni muhimu akachukua hatua za tahadhari mapema ili kukabili tatizo hili.
Gari kuwaka moto kunaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, fuatilia makala hii kwa karibu ili ufahamu mambo 9 yanayosababisha gari kuwaka moto na jinsi ya kuyaepuka.
1. Kuvuja kwa mafutaIkiwa gari litavuja mafuta ni rahisi sana kuwaka moto. Kumbuka mafuta ya gari pamoja na mafuta lainishi (oil) ni rahisi sana kushika moto.
Tafiti mbalimbali za ajali zimebaini kuwa kuvuja kwa mafuta ni chanzo kikubwa cha magari kuwaka moto.
Ni muhimu kuhakikisha unazingatia matengenezo na ukaguzi wa mara kwa mara wa gari lako ili kubaini kama kuna mahali panapovuja mafuta parekebishwe.
2. Hitilafu ya umemeGari lina mfumo wake wa umeme ambao unatakiwa uwe salama na ufanye kazi jinsi ipasavyo. Mfumo wa umeme unapokuwa na hitilafu, unaweza kusababisha cheche za moto na kusababisha gari kuwaka moto.
Ni muhimu kuhakikisha unatafuta mtaalamu wa magari akague na kurekebisha mfumo wa umeme wa gari lako kila mara. Pia ni muhimu kutumia vifa bora vya mfumo wa umeme wa gari, kwani vifaa duni vinaweza kusababisha moto.
3. Moto uliowazi (naked flame)Kama ambavyo moto ulio wazi ni hatari kwenye nyumba, ndivyo pia ilivyo kwenye gari. Kuwasha vitu kama vile sigara ndani ya gari kunaweza kusababisha ajali ya moto.
Ni muhimu kuepuka matumizi ya sigara au kubeba vitu vinavyoshika moto kirahisi ndani ya gari.
4. Gari kupata moto sana
Gari halitakiwi lipate moto kupita kiasi. Ikiwa sehemu za gari zitapata moto kupita kiasi zinaweza kuyeyuka au kuwaka moto.
Inashauriwa kuhakikisha mfumo wa kupooza gari uko katika hali nzuri. Pia ni muhimu kupumzisha ghari mara kwa mara wakati wa safari ndefu ili lipoe.
5. AjaliMsuguano unaweza kusababisha moto. Gari linapogongana na gari jingine au kugonga kitu kingine, linaweza kuzalisha cheche ambazo zitasababisha gari lishike moto.
Hivyo ni vyema kuzingatia kanuni za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
6. Hitilafu ya kimuundoKuna wakati matatizo ya kimuundo ya gari yanaweza kusababisha gari kuwaka moto. Hata hivyo, kutokana na matatizo ya kimuundo kuhusiana zaidi na watengenezaji, tatizo la kimuundo linapobainika hurekebishwa mara moja na watengenezaji.
Ni muhimu kununua gari kutoka kwa watengenezaji wanaoaminika na wenye uzoefu ili kuepuka hitilafu za kimuundo.
7. Matengenezo duniKama jinsi ambavyo umekwisha kuona kwenye hoja zilizotangulia hapo juu, ni muhimu sana kuzingatia swala la matengenezo. Mifumo ya gari kwa ujumla inahitaji matengenezo sahihi na kwa wakati.
Kwa mfano ikiwa hutozingatia matengenezo ya magurudumu, yanaweza kupasuka au kuwaka moto. Ni muhimu pia kuhakikisha mafuta lainishi (oil) yapo kwa kiwango kinachotakiwa ili kuepusha msuguano wa vyuma unaoweza kusababisha moto.
8. Vifaa vya nyongezaWatu wengi hupenda kuongeza vifaa mbalimbali kwenye magari yao tofauti na vile vilivyotoka kiwandani pamoja na gari. Vifa hivi huweza kuwa taa, redio, mifumo ya ulinzi, n.k. Vifaa hivi vya nyongeza vingi havina ubora na havifungwi na wataalamu.
Hivyo mara nyingi vifaa vya nyongeza kwenye magari vinaweza kusababisha gari kuwaka moto. Ni muhimu kuhakikisha ubora wa kifaa pamoja na kuhakikisha ufungwaji sahihi na salama.
Neno la mwisho
Tahadhari kabla ya hatari ni muhimu. Ni wazi kuwa ajali nyingi za magari kuwaka moto kwa sehemu kubwa huchangiwa na mambo yaliyoelezwa hapo juu. Ni muhimu tena sana kuzingatia matengenezo sahihi pamoja na kanuni muhimu za matumizi ya vyombo vya usafiri ili kuepusha ajali.