Mambo Yanayosababisha Baadhi ya Watoto Wasifanye Vizuri Kwenye Masomo



Mara kadhaa imeshuhudiwa baadhi ya watoto wakishindwa kufanya vizuri kwenye masomo. Jambo hili siyo zuri kwani linaathiri maisha ya watoto wenyewe pamoja na wazazi au walezi.

Wakati mwingine swala hili limekuwa kubwa kiasi cha kuwafanya baadhi ya watoto kupata shida hata kufanya mambo madogo kama vile kusoma na kuandika.

Hata hivyo kila jambo linalotokea duniani hutokea kwa sababu. Hivyo ukiwa wewe umeguswa na swala la baadhi ya watoto kutokufanya vizuri shuleni, basi karibu nikushirikishe mambo yanayosababisha baadhi ya watoto wasifanye vizuri kwenye masomo.

1. Matatizo ya kisaikolojia
Watoto wanaweza kukabiliwa na matatizo mbalimbali ya kisaikolojia ambayo huathiri uwezo wao wa kujifunza shuleni.

Baadhi ya watoto huzaliwa na matatizo haya huku mengine hutokana na matendo kama vile ukatili wa kijinsia au unyanyasaji mwingine wanaofanyiwa baadhi ya watoto ambayo hupelekea kuathirika kisaikolojia.

Baadhi ya watoto hubakwa, hulawitiwa, hupigwa, hunyimwa chakula au hata mahitaji muhimu. Hili huwasababisha washindwe kujifunza na kuelewa mara wanapokuwa shuleni.

2. Changamoto za kujifunza
Baadhi ya watoto hukabiliwa na changamoto za kujifunza kama vile kutokuweza kutambua namba na herufi, woga, kutokusikia au kuona vizuri, n.k.

Maswala haya huathiri mchakato mzima wa mtoto kujifunza na kusababisha ashindwe kufanya vizuri kwenye masomo.

3. Matatizo ya kifamilia
Baadhi ya familia ni ngumu sana kwenye swala la malezi ya watoto. Kuna familia ambazo kila siku ni ugomvi, ulevi, au hata unyanyasaji mwingine kama vile utumikishaji wa watoto pamoja na mazingira duni ya kuishi.

Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa watoto wanaoishi kwenye familia za aina hii huathirika kiakili, kimwili na hata kiroho, hivyo hushindwa kufanya vizuri kwenye masomo.

Hebu fikiri mtoto anayeishi kwenye familia ambayo kila siku ni ugomvi au inamazingira ya ulevi na uasherati, je ataweza kufanya vizuri kwenye masomo kweli? Naamini hapana.

4. Maradhi
Maradhi huathiri watu wa kila rika, lakini humwathiri mtoto zaidi. Maradhi yanapomkabili mtoto humfanya ashindwe kutulia na kujifunza vizuri mara awapo darasani.

Baadhi ya watoto hukabiliwa na maradhi ya akili, maradhi ya kurithi au kuambukizwa au hata ulemavu mbalimbali, hivi kwa pamoja huathiri mtoto na kumfanya asifanye vizuri kwenye masomo.

5. Shule duni
Siyo kila shule inafaa kwa ajili ya kila mtoto. Baadhi ya shule huendeshwa kwa lengo kuu la kupata pesa na si kuwawezesha watoto kufikia malengo yao.

Shule bora inapaswa kuwa na mazingira bora ya kujifunza pamoja na mikakati mbalimbali inayowezesha wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo.


6. Ukosefu wa nidhamu
Baadhi ya watoto huwa na nidhamu mbaya mara wanapokuwa shuleni; wengi hawatambui kuwa nidhamu ni msingi wa mafanikio katika taaluma.

Baadhi ya watoto au wanafunzi hutoroka, huvuta bangi, hulewa, huenda disko, n.k.

Wanafunzi hawa mara nyingi hawawi kwenye eneo husika kwa wakati husika, muda wa darasani wao wapo bwenini au nje ya shule, muda wa mitihani wao wapo eneo jingine au wanafanya jambo jingine. Hili huwafanya washindwe kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Hitimisho

Swala la kufanya vizuri kwenye masomo linahitaji pande kuu tatu zihusike kikamilifu yaani mzazi, mwanafunzi na shule ili liweze kutimia.

Ikiwa upande mmoja hautakaa kwenye nafasi yake jinsi ipasavyo ni lazima kiwango cha kufaulu cha mtoto kitakuwa duni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad