Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni, kupitia Chama cha Mapinduzi, Abbas Tarimba amesema kuwa yeye na Askofu Gwajima, wamejipambanua kwamba wanataka kwenda kuwatumikia wananchi na siyo kufuata mishahara na kwamba hata kama wakiondoka basi waache alama.
Kushoto ni mgombea Ubunge Jimbo la Kawe, Askofu Gwajima, na kulia ni Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni Abbas Tarimba.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 23, 2020, wakati akizungumza kwenye Ibada ya Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, Ubungo jijini Dar es Salaam na kuwaomba waumini kwenda kuwasemea yaliyo mazuri kwa ndugu zao ili mwisho wa siku waweze kuwachagua na kupata ushindi wa kishindo.
“Najua ninyi mlioko hapa na marafiki zenu mliopo nje ya hapa kila mmoja wenu akiwa na watu 10 tu nina uhakika siyo suala la ushindi tunalolilalamikia bali tunataka ushindi wa kishindo, mimi nitamuunga mkono Askofu na nitahangaika naye, na nyie ndugu zangu wa Kinondoni najua mna marafiki kule katusemeeni kwa wema, sisi ajenda yetu ni kutumikia wananchi na hatufuati mshahara” amesema Tarimba.
Kwa upande wake Askofu Gwajima amesema kuwa mwaka huu Kawe na Kinondoni patachimbika na kwamba wao hawajawahi kushindwa.