MWAKA jana mbunifu wa mavazi nchini; Martin Kadinda, aliwahi kusema kuwa, asilimia kubwa ya wasanii wa kiume Bongo, hawajui kuvaa.
Hii yote ni kutokana na wao wenyewe kuamini kuwa, wanaweza kujivalisha wakati hawawezi. Jambo linalofanya waonekane vituko pindi wanapoenda kwenye matukio makubwa.
“Wapo wasanii wengi na wana majina makubwa, wenyewe wanajiamini, acha wabaki hivyohivyo na hasa wasanii wa kiume ndiyo wanaharibu kabisa, bora hata wa kike,” alisema Kadinda.
Mbali na maneno ya mbunifu huyo, lakini wapo baadhi ya wasanii ambao wanajitahidi kuvaa vizuri na kupendeza, hata wanapokuwa kwenye ‘red carpet’ huwa na muonekano mzuri wa kuvutia.
Miongoni mwa wasanii hao ni pamoja na hawa ambao Uwazi limewafuatilia kwa muda mrefu kuhusu uvaaji wao na kujilidhisha kuwa, angalau wanatokelezea:
JUMA MUSSA (JUX)
Huyu ni msanii anayefanya poa kunako gemu ya muziki wa Bongo Fleva. Mwili wake na jinsi kifua chake kilivyokaa, huwachanganya baadhi ya watoto wa kike mjini.
Lakini kingine kinachombeba ni “Kulipuka”. Kusema kweli jamaa anajua kupangilia mavazi yake na kumfanya aonekane bomba anapojitokeza kwenye shughuli mbalimbali.
Akiwa kwenye red carpet, ndipo utampenda kwa sababu hautachoka kumwangalia. Shabiki yake mmoja aliyejitaja kwa jina la Shamim mkazi wa Masaki jijini Dar, aliyefanya mahojiano na Uwazi hivi karibuni, alisema: “Jux anajua kuvaa hadi anakera.”
Mbali na huyo, Jux amekuwa ndiyo msanii ambaye ametajwa mara kadhaa na wasanii wenzake kuwa ni staa ambaye akili zake nyingi huzielekeza kwenye mavazi ili aweze kwenda sambamba na biti za fasheni za kisasa.
OMARY NYEMBO (OMMY DIMPOZ)
Ni msanii wa muziki wa kizazi kipya Bongo, amewahi kunukuliwa akisema yeye ni bora asile, ila anunue mavazi.
Na kweli pekuapekua ya wachunguzi wetu kuhusu mavazi, imebaini kuwa mshikaji ni miongoni mwa wasanii wa kiume Bongo ambaye anajua kutupia vitu vya ukweli mwilini na kutokelezea kwenye ‘iventi’ mbalimbali.
Ni msanii ambaye anajua kupangilia vizuri mavazi yake na akapendeza, anajua kwenda na wakati, yaani nini avae na kwenye tukio gani.
Mara nyingi akitupia pamba mwilini mwake, hugeuka kuwa shabaha ya macho ya warembo kila anapokwenda.
HEMED SULEIMAN (PHD)
Ni msanii wa filamu na muziki wa Bongo Fleva. Mara nyingi ukimuona ndani ya suti utapenda, maana zinamkaa balaa.
Kifupi ana ‘damu ya nguo’, rangi yake nyeupe na mwili wake mkubwa, ndivyo vitu vinavyozidi kumbeba.
Ni miongoni mwa wasanii wanaojua kuvaa na kupendeza, kama unabisha kuhusu uchunguzi wetu, toa hoja ni lini jamaa umemuona kitaa akawa kaangushwa na mavazi aliyovaa?
SAID SEIF ALLY (NEDY MUSIC)
Msanii chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva, ambapo mwaka 2018 alishinda Tuzo ya All Africa Music Awards (Afrima) katika kipengele cha African Fans Favourite.
Ni msanii wa kiume Bongo ambaye naye anaingia kwenye orodha ya baadhi ya wasanii wa kiume wanaojua kutupia pamba kali.
Ukimwangalia, dogo ana umbo fulani dogodogo na la kuvutia, akitupia vyake mwilini, utampenda. Msanii huyu anajua kupangilia rangi za mavazi yake kulingana na mtoko wa siku husika. Si vibaya kumuita miongoni mwa mastaa wa mavazi kwa wasanii wa kiume Bongo.
NASIBU ABDUL (DIAMOND)
Ni msanii mkubwa wa Muziki wa Bongo Fleva ndani na nje ya nchi. Siku hizi jamaa amekuwa mcharo kwelikweli, ule ushamba wa Mbagala aliochekwa nao enzi anaanza kutoka, ni kama ameuzika.
Mondi siku hizi ni mtu wa tizi kinomanoma, anatengeneza mwili ili aonekana ‘hendisamu’ kwa wadada wa mjini.
Ukimwa ngalia siku hizi kila anapotoka, utagundua kuwa jamaa ana mapigo fla’ni hivi ya kichokozi hasa kwa warembo wa mjini.
Jamaa ana katalogi zake za mbele, maana hata akivaa shati, hafungi vifungo vyote hapo akitupia na suruali yake ya kubana mwili kidogo, anato kelezea kinoma.
Kila akitokeza kwenye shughuli, utasikia wadada wa mjini “Jamani kapendeza” kuonesha kuwa mavazi yake yaliwashika panyewe wenye macho yao ya kidakudaku.
HITIMISHO
Makala haya siyo msaafu kwamba hauwezi kubadilika, ni mtazamo tu wa mwandishi na uchunguzi wa Uwazi; wewe ukiwa na jicho lako na umeona kuna msanii mwingine hakosei kwenye ishu ya pamba, tupia maoni yako kupitia namba hii ya simu 0714 895 555.
MAKALA: MEMORISE RICHARD