Mbeya: Hofu Yatanda Mwalimu Kuchinjwa Shingo!



HOFU kuu imetanda wilayani Kyela mkoani Mbeya kufuatia tukio la kutisha la mauaji ya Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Ipinda, Hemed Mwipopo (54).


Mwalimu Mwaipopo alikuwa mkazi wa Kitongoji cha Mpanga Kijiji cha Mapunguti Kata ya Ikama.

Habari zilizopatikana zilidai kuwa, mwalimu huyo aliuawa kwa kuchinjwa shingoni na watu wasiojulikana wiki iliyopita kwa sababu zisizofahamika.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mpunguti, Suma Mwaifwani aliliambia gazeti hili kuwa, Mwalimu Mwaipopo enzi za uhai wake, alikuwa akifundisha Shule ya Mwenge iliyopo Ipinda, huku familia yake ikiishi Kyela mjini.


Mwaifwani alisema kuwa, Mwalimu Mwaipopo alijenga nyumba katika Kijiji cha Mpunguti kwa ajili ya kazi zake za ujasiriamali, kikiwemo kilimo.

Alisema kifo cha Mwalimu Mwaipopo kimewashangaza wengi kijijini hapo, baada ya mwili wake kukutwa ukiwa umechinjwa shingoni, hali iliyozua taharuki kwa baadhi ya wakazi wa kata hiyo.

Henry Wambua ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Ipinda wilayani Kyela, ambaye alithibitisha kuupokea mwili wa Mwalimu Mwaipopo na kuuhifadhi mochwari kabla ya kuukabidhisha kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

Alisema kuwa, wakati mwili huo unafikishwa hospitalini hapo, ulikuwa umekatwa sehemu ya koromeo na kitu chenye ncha kali.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa, awali mwalimu huyo alikuwa na kesi ya kujenga ghala la kuhifadhia mazao, ambapo hatua tano za ujenzi huo, zilidaiwa kuvuka au kuingia kwenye eneo la barabara ya kijiji.


Alisema kuwa, kufuatia madai hayo, uongozi wa kijiji ulimshtaki katika Baraza la Ardhi la Kata.


Hata hivyo, alisema, katika kesi hiyo, Mwalimu Mwaipopo alishinda, ndipo baada ya siku kadhaa, yakatokea mauaji hayo.


Kamanda Matei alisema kuwa, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watu watano, akiwemo mwenyekiti wa kitongoji kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.

Kamanda Matei alitoa rai kwa wasuluhishi wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata kuwa makini katika utoaji wa haki ili kuondoa matatizo kama hayo.


Pia alitoa katazo kwa wananchi kujichukulia sheria mkononi, akisema wamekuwa wakitoa elimu hiyo na wataendelea kutoa ili vitendo hivyo visijitokeze.

Naye Claudia Kitta, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya alisema kuwa, tukio hilo limewashangaza wengi, hivyo kuwataka wananchi kuacha mara moja kujichukulia sheria mkononi.


“Ninalaani vikali mauaji haya ya kikatili,” alisema Kitta ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kyela.

Aliongeza kuwa, matukio kama hayo, yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara licha ya wao kutoa elimu kupitia mikutano na vyombo vya habari na kwamba, anawaasa wananchi wafuate sheria zilizopo kwa mtu aliyefanya kosa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na si kuchukua sheria mkononi.


Mwalimu Mwaipopo alizikwa wiki iliyopita kijijini hapo, ambapo ameacha mjane na watoto.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad