MFALME wa zamani wa Uhispania, Juan Carlos, ameamuwa kuihama nchi yake katika uamuzi wa aina yake unaolenga kuunusuru ufalme baada ya mkururo wa tuhuma za ufisadi dhidi yake na wakati waendesha mashitaka wakimchunguza.
Tamko la kasri ya kifalme lililotolewa jana (Agosti 3) lilinukulu barua ya Juan Carlos kwa mwanawe na mfalme wa sasa, Filipe, akisema kwamba anataka kumuwezesha mwanawe huyo kuongoza kwa salama licha ya hasira za umma juu ya masuala ya maisha yake binafsi.
“Nikiongozwa na hamu yangu binafsi ya kufanya kile kilicho bora zaidi katika kuwatumikia watu wa Uhispania, taasisi zake na wewe kama mfalme, ninakufahamisha uamuzi wangu huu wa kuondoka Uhispania wakati huu.” Sehemu ya barua hiyo ilisema.
Mwanawe, Mfalme Filipe, alimshukuru kwa uamuzi wake huo, akisisitiza umuhimu wa kihistoria wa baba yake kwenye “demokrasia ya Uhispania.”
Mfalme huyo aliyewahi kuwa mashuhuri sana nchini mwake na ambaye bado anatumia jina la Mfalme Mkuu, aliripotiwa kwamba tayari ameshaondoka Uhispania, ingawa vyombo vya habari vya huko havijasema alipokwendea.
Hata hivyo, televisheni moja ya Ureno, TV124, na gazeti la udaku la Corrieo da Manha yameripoti kwamba Juan Carlos yupo kwenye mji wa kifahari wa Cascais karibu na mji mkuu wa Ureno, Lisbon, ambako aliwahi kuishi akiwa mtoto. Hata hivyo, vyombo hivyo havikutaja chanzo cha habari hiyo.
Juan Carlos aliingia madarakani mwaka 1975 baada ya kifo cha Jenerali Francisco Franco na alikuwa akiheshimiwa sana kutokana na jukumu lake la kuiongoza Uhispania kutoka kwenye udikteta kueleka utawala wa kidemokrasia.
Hata hivyo, heshima yake ilianza kuporomoka baadaye kutokana na mkururo wa kashfa zilizomfanya astaafu mwaka 2014. Wakili wake, Javier Sanchez-Junco, alisema licha ya kuondoka kwake, mfalme huyo wa zamani ataendelea kuwa kwenye mikono ya ofisi ya mwendesha mashitaka muda wowote itakapomuhitajia.
Kwa wiki kadhaa sasa, shinikizo limekuwa likiongezeka kwa wote wawili, baada ya waendesha mashitaka wa nchi hiyo na wa Uswisi kuanza kuchunguza tuhuma za rushwa dhidi yao.
Gazeti la La Tribune de Geneve la nchini Uswisi liliripoti mnamo mwezi Machi kwamba Juan Carlos alikuwa amepokea dola milioni 100 kutoka kwa aliyekuwa Mfalme wa Saudi Arabia kama rushwa kwa mradi wa reli iendayo kwa kasi.
Baadaye magazeti ya nchini kwake yalidai kwamba sehemu kubwa ya fedha hizo alimpa hawara wake wa zamani. Kawaida wafalme wa Uhispania wana kinga ya kutokushitakiwa, lakini kuachia kwake madaraka mwaka 2014 kulimuondolea Juan Carlos kinga hiyo.
Kwa vyovyote vile, uamuzi huu wa kuhama nchi unatazamiwa kuwagawa tena Wahispania kati ya wale wanaomuunga mkono na wanaompinga, huku wanaompinga wakitaka asalie nchini kubaliana na mashitaka na wale wanaomuunga mkono wakidhani kwamba ni jambo sahihi kwa mfalme huyo wa zamani kuhama nchi aliyoiongoza kwa miaka takribani miongo minne.