Mgombea Asiyekuwa na ‘Jinsia Yoyote’ Afunguka Mazito – Video


Dar: Baby John (26) mkazi wa Kivule-Msongola wilayani Ilala jijini Dar es Salaam ambaye hivi karibuni aligombea uteuzi wa nafasi ya Ubunge kupitia Viti Maalum Walemavu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujitangaza mbele ya wajumbe kuwa yeye ni mlemavu kwa kuwa ni binadamu aliyezaliwa bila kuwa na jinsia yoyote, amefunguka mazito, Gazeti la IJUMAA limepiga naye stori ndefu.



Akizungumza ana kwa ana na mwandishi wetu, Baby alisema anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kukubaliana na hali hiyo ambayo amezaliwa nayo.



“Unajua kumtumaini Mungu kuna faida kubwa, maana tatizo langu kama mtu usipokuwa na moyo unaweza kumkufuru Mungu, maana linafikirisha mno hata kumsimulia mwingine,” anasema Baby.



ALIGUNDULIKAJE?

Baby anasema kuwa, alipozaliwa ulizuka utata kwa madaktari waliokuwa wakimhudumia kuhusiana na jinsia yake ambapo wengine walisema yeye ni wa kike na wengine walimwambia mama yake kuwa amejifungua mtoto wa kiume.



“Hadi mama anaruhusiwa kurudi nyumbani bado alikuwa hajui mimi ni mtoto wa jinsia gani kutokana na maumbile yangu yalivyokuwa yanaonekana.



“Baadaye kuna daktari mmoja alimwambia mama yangu kuwa mimi ni mtoto wa kike, tangu hapo mama akaanza kunilea kama mtoto wa kike, lakini sikuwa na maumbile ya siri ya kike.



“Nilikaa katika uangalizi wa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake nikiangaliwa kwa ukaribu afya yangu na maenedeleo ya ukuaji wangu.

“Wazazi wangu waliendelea kunilea kama mtoto wa kike tena kwa umakini na usiri ili watu wengine wasielewe tatizo langu.



“Mara kadhaa wazazi wangu waliponipeleka kliniki na kufanyia vipimo sikuonesha viashiria vyovyote kuwa mimi ni mtoto wa kike au wa kiume,” anasema Baby.



Aliongeza kuwa, alipofika umri wa kuanza Darasa la Kwanza alikwenda shule kama mwanafunzi wa kike na kwamba muda mwingi aliweza kujilinda asigunduliwe na wenzake kwa kutumia mbinu alizofundishwa na mama yake.



“Hakuna aliyeweza kunigundua hadi nilipomaliza Darasa la Saba na kufanikiwa kwenda kitato cha kwanza ambako nako niliendelea kutunza siri yangu hadi nilipomaliza.



“Ingawa nilisoma shule ya bweni niliweza kutunza siri yangu, ilikuwa ni heri kuvaa nguo nikiwa juu ya kitanda changu cha juu kuliko mtu anione.



“Kingine nilikuwa sitaki kuchangamana na wasichana wenzangu pale shuleni, hata ikitokea tunakwenda kuoga mimi nilikuwa naoga nikiwa nimevaa nguo za ndani.



“Nimeishi maisha hayo miaka yote hiyo bila kugundulika hadi nilipoamua mimi mwenyewe kujiweka wazi mbele ya jamii kwa sababu nimekubalina na hali niliyo nayo,” anasema Baby.



Aliongeza kuwa, ingawa muonekano wake ni kama mwanamke, lakini hajawahi kuingia kwenye siku zake, wala hana hisia zozote za mapenzi.



“Kutokana na changamoto ambayo niko nayo kuna kipindi nilitamani kabisa kujiua, lakini Mungu akanitetea, kwa sababu mimi najua wazi siwezi kuwa na mwanaume, siwezi kuzaa wala kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanaume kwa sababu kwenye uhusiano lazima kushiriki tendo la ndoa.



“Sasa mimi haiwezekani kushiriki tendo hilo kwa sababu sina sehemu ya kuniwezesha kukutana kimwili na mwanaume,” anasema Baby.



Akifafanua kuhusu maumbile yake ya sehemu za siri alisema yapo kwa ajili ya kumuwezesha kupata haja kubwa na ndogo na siyo vinginevyo. Alisema, pamoja na kuwa kwenye changamoto hiyo kubwa, bado hajakata tamaa za kutimiza ndoto zake za kimaisha.



“Siwezi kukata tamaa, napambana. Hivi sasa niko shule nasomea mambo ya ufamasia (masuala ya madawa, kitaalam ni Famasia) nimepanga kuwasaidia watu ambao wanachangamoto kama zangu,” anasema Baby.



Baby alijitangaza hadharani wakati wa mchakato wa kuomba kura kwa wajumbe ili aweze kupata ridhaa ya kugombea Ubunge wa Viti maalum kupitia nafasi za Walemavu ambapo kwa bahati mbaya kura zake hazikumuwesha kushinda.



Stori: Imelda Mtema. Ijumaa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad