Rais wa Lebanon Michel Aoun amesema kuwa mlipuko uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 150 na kufanya uharibifu mkubwa mjini Beirut huenda ulisababishwa na uzembe au shambulio kutoka nje.Kupitia hotuba aliyoitoa kwa runinga, Rais Aoun amesema inawezekana tukio hilo lilisababishwa na uzembe au shambulio la roketi.
Hata hivyo, Ofisi yake imesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha mlipuko huo unaendelea.Aoun amemtaka Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliyeitembelea Beirut jana Alhamisi, kuhifadhi picha za anga katika eneo la tukio ili kubaini kilichotokea na iwapo Ufaransa haitakuwa na picha hizo za anga, amesema ataziulizia kutoka sehemu nyengine.
Aoun ameahidi kufanyika kwa uchunguzi kamili juu ya tukio hilo huku tayari maafisa 20 wa bandari wakikamatwa kama sehemu ya uchunguzi huo.Benki kuu nchini humo imesema imezizuia akaunti za washukiwa saba, akiwemo wakuu wa bandari na forodha.