Morrison Ateka Shoo Mazoezi Simba Sc


TIMU ya SIMBA jana Jumatatu jioni Agosti 17, 2020 ilianza rasmi mazoezi yanayofanyika kwenye Uwanja wao wa Mo Simba Arena uliopo Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam huku winga wao mpya aliyetokea Yanga Sc kwa mkataba wa miaka miwili, Bernard Morrison akiwa kivutio mazoezini hapo.

Kwa mujibu wa Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyotolewa jana na Bodi ya Ligi, Simba watafungua dimba la Ligi Kuu Bara Septemba 6, mwaka huu wakiwa ugenini Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya Ihefu FC iliyopanda daraja msimu huu.


Morrison amekuwa gumzo tangu kutua kambini na kwenye mazoezi hayo kwa mashabiki wanaoshuhudia mazoezi yao ambao wamesikika wakizungumzia kiwango chake na uwezo wake ndani ya Simba.

Kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu na Simba, Morrison amekuwa gumzo kutokana na sakata lake la mkataba baina yake na Yanga ambapo aliishitaki klabu yake ya zamani kuwa wameghushi saini yake lakini Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilimpa ushindi baada ya kubaini mapungufu katika mkataba wake na Yanga.


Hata kamati hiyo ilimpeleka Morrison kwenye Kamati ya Maadili kwa kosa la kusaini mkataba Simba wakati shauri la kesi yake halijamalizika.

Wachezaji wengine wapya waliosajiliwa msimu huu waliofika mazoezini ni Joash Onyango, Charles Ilanfya, Chris Mugalu, Ibrahim Ame, Larry Bwalya na David Kameta ‘Duchu’.


Wakati wachezaji wapya wakiwepo, nyota wa zamani wa kikosi hicho Meddie Kagere , Clatous Chama, Luis Miquissone, Francis Kahata, Shomari Kapombe na Paschal Wawa hawakuwepo.

Simba ilianza mazoezi kwa kufanya mazoezi mepesi ya kunyoosha viungo na baada ya hapo walipangiwa koni na kuanza kuchezea mpira kwa kupigiana pasi.

Mazoezi hayo huwa yanatumika kama kupasha misuli kwa wachezaji badala ya kukimbia kuzunguka uwanja. Wachezaji wa zamani waliokuwepo ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salim, Gadiel Michael, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Said Ndemla, John Bocco, Ibrahim Ajibu, Mzamiru Yassin, Miraj Athuman na Gerson Fraga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad