Msemaji Mkuu wa Serikali: Vijiji vyote Tanzania kupatiwa umeme ifikapo Juni 2021



Tanzania inalenga kuweka rekodi ya kusambaza umeme katika vijiji vyote zaidi ya 12,000 nchini ifikapo Juni 30, 2021.


Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na vyombo vya habari akielezea mafanikio ya serikali katika sekta ya madini na nishati ndani ya miaka mitano iliyopita.


Dkt. Abbasi amesema kuwa kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa na umeme ni 2,018, lakini kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 jumla ya vijiji vilivyounganishwa umeme ni 7,314, hatua ambayo amesema ni historia.


“Hadi Juni 30, 2021, vijiji vyote zaidi ya 12,000 vinatarajiwa kuwa na umeme,” amesema Dkt. Abbasi huku akieleza kuwa uamuzi utabaki mikononi mwa wananchi kuamua kuweka umeme kwenye nyumba zao au kutokuweka.


Akitaja mafanikio mengine katika sekta ya nishati amesema ni pamoja na TANESCO kuanza kujiendesha yenyewe bila kutegemea ruzuku serikali.


Amesema shirika hilo pia limeacha kutumia mitambo ya kukodi na kuokoa shilingi bilioni 118 kwa mwaka ambazo zingelipwa kama ‘capacity charge’ bila kujali kama mitambo inafanya kazi au la.


Ameongeza kuwa kwa miaka mitano, serikali imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,308 hadi 1,600 ambapo jumla ya shilingi trilioni 1.109 zimetumika kwenye miradi mbalimbali inayolenga kuzalisha umeme kutoka vyanzo mbalimbali.


Katika kipindi hicho amebainisha kuwa nguvu kubwa imewekezwa kwenye umeme wa gesi.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad