YANGA juzi imeanza mazoezi rasmi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, 2020/2021, kwa kufanya program tatu kwa siku katika kukiimarisha kikosi chao katika kuelekea msimu huo mpya.
Timu hiyo ilianza mazoezi yake na wachezaji wake wawili kati ya wanne waliowasajili ambao ni Waziri Junior aliyekuwa anakipiga Mbao FC na Yassin Mustapha wa Polisi Tanzania, huku Bakari Mwamnyeto na Zawadi Mauya wakiwa na ruhusa maalum.
Katika kuelekea msimu ujao, Yanga imepania kufanya vema ikiwemo kutwaa ubingwa wa ligi iliyoukosa kwa misimu mitatu mfululizo ambayo yote imekwenda kwa watani wao, Simba.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa timu hiyo imepanga kuanza kufanya program tatu za mazoezi kwa siku.
Bumbuli alisema kuwa lengo ni kuhakikisha wanarejesha fitinesi ya wachezaji baada ya kutoka likizo kwenye mapumziko ya wiki mbili waliyowapa wachezaji wao.
Aliongeza kuwa program hiyo wataifanya kwa asubuhi kufanya mazoezi ya uwanjani, mchana gym na jioni wanarudi tena uwanjani kwa ajili ya kuwapa mbinu za uchezaji.
“Muda ni mchache tuliokuwa nao kabla ya ligi kuanza Septemba 6, mwaka huu hivyo ni lazima tufanya program hizo za mazoezi baada ya kocha Riedoh Berdien kupendekeza.”Hivyo, leo (juzi) tumeanza mazoezi madogomadogo kabla ya kesho (jana), ambako timu itaanza mazoezi ya nguvu kwa kufanya mazoezi mara tatu kwa siku.
“Kocha amependekeza timu ifanye program tatu za mazoezi asubuhi ya uwanjani, mchana tutakuwa tunafanya mazoezi ya gym kabla ya jioni kufanya mazoezi ya kimbinu uwanjani.
“Kocha amependekeza hivyo kutokana na muda kutubana, hivyo ni lazima vitu vyote viwili vifanyike ndani ya wakati mmoja kwa maana ya kuwafanyisha mazoezi ya fitinesi na kimbinu ndani ya wakati mmoja,”alisema Bumbuli.