Mwanamke Akatwa Mikono na Mume Wake, Aeleza ilivyokuwa


Wiki chache zilizopita, Purity alikuwa na mikono yake miwili kabla ya kushambuliwa na mume wake.

Tahadhari: Baadhi ya maneno huenda yakaogofya

Alikimbilia nyumbani kwa baba yake baada ya ugomvi wa nyumbani lakini mumewe akamufuata huko akidai kutafuta suluhu.



Alimshawishi baba yake Purity akimtaka azungumze na binti yake, lakini mkewe akakataa na kujifungua kwenye chumba chake cha kulala kwao.

Purity akionekana mwenye kutaka kububujikwa na machozi anasema,

”Baba yangu alitoka akaenda, jamaa akaanza kuniita tuongee. Mimi nilikwambia sitaki story zake na sijui amekuja hapa kwetu kufanya nini? Akaniambia ni sawa. Mimi nilikaa kwa room. nilikuwa nimelala. Hiyo sa akiniambia hivyo ilikuwa saa mbili saa tatu hivi. Alikaakaa kutoka saa nne, saa tano. Mi saa sita usiku ndio nilishitukia yuko kwa room yangu”.

”Alianza na kuninyonga, nikamwambia acha niamke, tukae chini tuongee, akaniambia yeye alikuwa ameamua kuniua ama yeye auawe. Ndipo alipoanza kunikatakata. Akanikatakata kichwa, akanikatakata mikono. Nilianza kupiga nduru, watu walikuja, watu waliambia jamaa afungue mlango, akafungua. Kutoka hapo sijui kulienda aje, nilijipata hospitali nikiwa sina mikono”.

Inasemekana mwanamume huyo alishambuliwa na umma hadi kufa. Purity sasa anapata matibabu na ushauri nasaha.

Ukatili dhidi ya wanawake umeongezeka nchini Kenya, hasa wakati huu wa janga la corona huku takwimu za serikali zikionesha kuwa wanawake wanne kati ya kumi wameathirika.

Aidha uongozi wa kaunti ya Makueni nchini Kenya umezindua makao salama ili kuokoa wanawake ambao wanaishi katika mazingira ya ukatili.

Mwanamke mwengine aliyekimbilia eneo hilo baada ya kupigwa na mume wake anasema:

”Sasa wakati alinichapa na akaona sitosheki na kupigwa ndio akaendea fimbo. Hapo kwangu kuna ovacado mbili, akachukua fimbo tunayochunia ovacado, akaingia nayo kwa nyumba na akafunga mlango. Wakati aliingia kwa nyumba ndio akanichapa hii mkono na mti. Na hii mkono ndio ilikuwa imeshika mtoto. Akasema anataka laini yake, na mimi sikuwa nimeachilia mtoto wangu. Nilikuwa nimeamua kama nikufa nikufe na mtoto wangu nikiwa na yeye”.

Kulingana na Umoja wa Mataifa masharti yaliyowekwa kuzuia maambukizi ya corona, yamesababisha maisha kuwa magumu kwa wanawake hasa nyumbani.

Ukosefu wa ajira na changamoto za kiuchumi zimesababisha hali kuwa ngumu kwa familia nyingi.

Makao salama kama yaliyojengwa ni mojawapo ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya kaunti ya Makueni kulinda wanawake.

Adelina Mwau naibu gavana wa kaunti ya Makueni amesema:

”Tulifikiria sana tutaiweka wapi, kwasababu haiwezi ikawekwa mahali popote pale. Kuna usaidizi wa kitengo cha ushauri. Hapo kuna usalama kwa wale wanaokuja wakiwa wamedhulumiwa. Wasifuatwe na waume zao. Ili wapate amani ya moyo”.

Uchunguzi wa kitaifa kuhusu visa vya ukatili dhidi ya wanawake umeanzishwa kama alivyoamuru rais. Na matokeo yake yakitarajiwa kutoa mapendekezo yatakayochangia kutafuta suluhu hasa kuhusu usalama wa wanawake nyumbani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad