MWANAMKE mmoja Mkazi wa Manzese Argentina jijini Dar es Salaam, Asha Juma amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili ya kumiliki risasi 45 kinyume cha Sheria.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Adolph Lema leo Agosti 12, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mmbando imedai Mei 17, 2020 katika eneo la Manzese jijini Dar es Salaam mshtakiwa Asha alikutwa akimiliki risasi 29 zenye kipenyo milimita 12 kinyume cha sheria ya usimamizi wa silaha na risasi nchini.
Katika shtaka la pili imedaiwa, siku na mahali hapo Asha alikutwa akimiliki risasi 16 zenye kipenyo cha milimita 9 kinyume na sheria ya usimamizi wa silaha na risasi.
Hata hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida zinasikilizwa Mahakama Kuu au kwa kibali maalimu kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi Agosti 26, mwaka huu. Mshtakiwa amepelekwa segerea.