POLISI nchini Nigeria wameumuokoa mwanamme mmoja aliyefahamika kwa jina la Ahmed Aminu mwenye umri wa mika 32 ambaye alifungwa na familia yake kwa miaka 30 kwa sababu alikuwa na ugonjwa wa akili.
Mtu huyo alikuwa amefungwa kwa miongo kadhaa huku miguu yake ikifungwa pamoja kwa chuma kilichoingizwa kwenye gogo la mti, ndani ya chumba ambacho hakikuwa na dirisha wala mlango, katika makazi ya familia yake huko Farawa, jimbo la Kano.
Majirani walitoa taarifa kwa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya mtandao wa haki za binadamu na baadaye polisi wakaitwa na kumkuta akiwa ana muonekano wa mifupa tu iliyokuwa imebaki mwilini mwake.
“Ana matatizo ya kiakili, alikuwa na fujo na badala ya kuomba msaada mwaka 1990 baba yake akaamua kuwa jambo bora la kufanya ni kumfunga,” alisema Shuaibu wa Shirika la Haki za Binadamu.
“Tulimkuta Aminu akiwa katika hali mbaya sana, alikuwa amefungwa sehemu moja tu ambayo alkuwa anajisaidia hapo na inawezekana hata bila kupewa chakula na anaonekana alikuwa anakaribia kufa muda wowote.
“Wakati baba yake alipokufa miaka kadhaa iliyopita kaka zake wawili, ambao ni wadogo zake, waliendelea kumfunga lakini leo amekuwa huru. Baadhi ya majirani walioifahamu hali yake ndiyo waliohusika katika uokoaji huu,” aliongeza.
Kwa sasa yuko katika Hospitali kuu ya Rogo ambako anapewa matibabu, huku kaka zake wakihojiwa na polisi. Huu ni uokoaji wa tatu wa hali ya juu katika kipindi cha wiki mbili wa watu wenye matatizo waliofungwa na familia zao katika eneo hilo la kaskazini mwa Nigeria.
Polisi wanasema myu huo alifungwa na wazazi wake kwa kushukiwa kutumia madawa ya kulevya na hivyo kuachwa bila kupewa huduma nzuri ya chakula wala afya.