KAMA kawa kama dawa, Mfalme wa Muziki wa Taarab Bongo, Mzee Yusuf anatarajia kuunguruma usiku wa Agosti 7, mwaka huu ukiwa ni mkesha wa Sikukuu ya Nanenane pale kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem jijini Dar.
Akizungumza na Championi Jumamosi, mratibu wa shoo hiyo, Rajab Mteta ‘KP’, alisema kuwa awali shoo hiyo ilitakiwa ifanyike Julai 31, mwaka huu, lakini kutokana na msiba mzito uliolikumba taifa wa kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, imesogezwa mbele.
“Niwaombe mashabiki wote wa Mzee Yusuf tukutane pale Dar Live Agosti 7, mwaka huu, Mzee anarudi mjini na ameahidi kufanya mambo ambayo hamjawahi kuyaona tangu ameanza kufanya muziki hadi pale alipoacha,” alisema KP.
Kwa upande wake Mzee Yusuf, amewataka mashabiki wake wafi ke kwa wingi kwenda kuona kile alichowaandalia baada ya kuwa nje kwenye game kwa muda mrefu.
“Naomba mashabiki wangu wafi ke kwa wingi, kama mnavyojua huwa sinaga kazi mbovu mjini, mfalme narudi, tena narudi kwa kishindo kikubwa, nimejipanga kuwapa burudani ya kutosha,” alisema Mzee Yusuf.
Kabla ya kuacha kuimba Taarab, Mzee Yusuf alikuwa tishio kwenye muziki huo ambapo ngoma zake kama Kaning’ang’ania, Mahaba Niue, Mpenzi Chocolate na Najiamini ambazo bado zinatamba mtaani mpaka sasa.