Dawa ya moto ni moto! Ndivyo unavyoweza kusema, kufuatia, Rais wa Kruu la Konde Gang, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kumuonesha bosi wake wa zamani, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ yeye si wa mchezomchezo kwa sasa.
Alichokifanya Harmonize au Harmo, baada ya Diamond au Mondi kuingia kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar na chopa siku ya shoo (Simba Day, Agosti 22), yeye aliamjibu kibabe kwa kuingia na usafiri huo wa gharama kwenye siku ya ‘kutesti’ mitambo badala ya shoo yenyewe (Siku ya Mwananchi).
“Huu ni zaidi ya ubabe, yaani Mondi aliona amekomesha kwa kuibuka na chopa siku ya shoo, Harmo akamjibu kwamba kwake hayo ni mambo madogo, anautumia usafiri huo kwenye mazoezi, siku moja kabla ya shoo,” alifunguka mtu wa karibu na timu ya Harmo alipozungumza na IJUMAA WIKIENDA baada ya mkali huyo kuibuka na usafiri huo kwenye Uwanja wa Mkapa, Agosti 28, mwaka huu
Mtu huyo aliyeomba hifadhi ya jina aliekwenda mbele zaidi kwa kusema, Harmo anazidi kumuonesha msuli Mondi kwani hata kabla ya juzi, huko nyuma aliwahi kutumia usafiri huo kwenye moja ya shoo zake. “Harmo asharuka na chopa sana tu sio leo tu. Alishawahi kufanya hivyo kule mkoani Mtwara mbona,” alisema.
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ ambaye alieleza jinsi wao walivyojipanga kufanya shoo nzuri na si kushidana na msanii yeyote. Mahojiano kati ya Mjerumani na IJUMAA WIKIENDA yalikuwa hivi;
IJUMAA WIKIENDA:
Tulitegemea kuona Harmo akiingia na helikopta kwenye shoo yenyewe, lakini akaingia nayo uwanjani wakati akienda kufanya sound-check na hii imezua maneno mengi mtandaoni, ni jambo ambalo mlilipanga kabla?
MENEJA:
Nafikiri kila mtu akiwa anataka kufanya kitu anakuwa na matamanio yake ya nini anataka kionekane pindi anapoenda kufanya jambo, kwa hiyo yeye kuingia na helkopta kwenye sound-chek ni kitu ambacho alitamani kukifanya.
IJUMAA WIKIENDA:
Vipi kuhusu gharama za kukodi ile helkopta ziko vipi?
MENEJA: Kuhusu gharama za kukodi hiyo nafikiri siyo jambo zuri kulijadili kwa sababu vitu vingi vina gharama nyingi hivyo mashabiki zake wajue tu kwamba amewekeza na huwa anawekeza sana kwa ajili ya kuwaburudisha.
IJUMAA WIKIENDA: Baada ya Harmo kumaliza kufanya sound-chek kulikuwa na maneno tofauti, wapo waliompongeza kwa alichokifanya na wengine wakamponda kuwa hana ubunifu kwa sababu amemuiga Mondi, wewe kama meneja una lipi la kuzungumza?
MENEJA: Sisi siku zote huwa hatufanyi kitu kwa kuangalia mtu f’lani kafanya nini, bali tunafanya kitu ambacho tunajua hiki mashabiki wetu watakipenda na kitatuongezea heshima na thamani kwa msanii wetu, kwa hiyo mashabiki wetu wajue kwamba hatufanyi kitu kushindana na mtu.
Tangu aondoke Wasafi mwishoni mwa mwaka jana, kumekuwa na ushindani mkubwa kati ya Harmo na Mondi kutoka kwa mashabiki wao, jambo ambalo linatajwa kuwa na tija kwenye kukua kwa muziki wa Bongo Fleva.