BEKI kisiki wa Klabu ya Barcelona, Gerard Pique, amesema kikosi chao kinahitaji mabadiliko makubwa kama wanahitaji kurejesha ubora wao.
Kauli hiyo inafuatia Barcelona kutandikwa vilivyo na Bayern Munich kwa jumla ya mabao 8-2 katika mchezo wa robo fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya uliopigwa usiku wa jana.
Raia huyo wa Hispania mwenye umri wa miaka 33, amesema hata yeye yupo tayari kuwa mchezaji wa kwanza kuondoka kuruhusu mabadiliko hayo iwapo Klabu itabariki.
Pique ambaye katika miaka yake 12 akiwa na Barcelona ameshinda mataji 20, ameongeza kuwa wanapaswa kuwajibika akianza kocha na kisha wachezaji wafuatie.
Nyota huyo amesema ni vyema wachezaji wakatafakari na kufanya uamuzi ulio bora kwa maisha yao lakini zaidi kwa Klabu hiyo ambayo imekuwa na ushindani mkubwa kwa miaka mingi barani Ulaya.
Barcelona inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa viongozi mwakani (2021) huku ikiaminika kwamba itakuwa ngumu kwa Rais wa sasa, Jose Maria Bartomeu, kurejea madarakani kutokana na mporomoko mkubwa wa klabu hiyo kwa miaka ya karibuni.