Polisi Yafafanua Kisa cha Mbunge Sugu Kukamatwa



MGOMBEA wa Ubunge Jimbo la Mbeya Mjini kupitia CHADEMA Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu pamoja na wanachama 15 wa chama hicho wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya maandamano ambayo ni kinyume na sheria.

Majira ya saa sita mchana, leo Agosti 14, 2020, wafuasi wa CHADEMA pamoja na Mgombea Sugu walifika katika ofisi cha chama hicho zilizopo Kata ya Sinde kwa lengo la kuanza pamoja safari ya kumsindikia katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge Jimbo la Mbeya Mjini.


Jeshi la Polisi lilifanya ufuatiliaji wa zoezi hilo na kubaini kuwa yalikuwa ni maandamano ambayo hayana kibali chochote kutoka kwao na kwamba ni kunyume na sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, amekiri Sugu na wenzake kukamatwa na kwamba lengo ni kupewa elimu juu ya mambo ya kuzingatia katika msimu huu wa kuelekea uchaguzi na kwamba wakati wa kufanya maandamano bado kwa sababu Tume bado haijatoa majina na kibali cha kuanza kufanyika kwa kampeni hivyo wangesubiri utaratibu.

“Nilipata taarifa kuwa Sugu leo anaenda kuchukua fomu kwa maandamano makubwa ambayo yalianzia Mitaa ya Sinde na wanachama hao waliamua kumsindikiza hadi ofisi za Tume licha ya kutopewa taarifa, lakini pia kulikuwa na vurugu ambazo wanachama walizifanya walipofika katika ofisi za NEC”, amesema Kamanda Matei.

Awali akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa zoezi la kukabidhiana fomu na kabla ya Sugu hajatiwa nguvuni, Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Ademe Ng’wanidako alisema alitimiza wajibu wake wa kumkabidhi fomu ili kwenda kuijaza na kutafuta wadhamini.


“Mimi zoezi langu tayari nimelitekeleza kwa kutoa fomu kwa mgombea kinachofuata akatafute wadhamini na kuzirejesha kuhusu kukamatwa kwa wafuasi wa chama hicho hizo ni habari nyingine”, alisema Mkurugenzi huyo.

Katibu wa CHADEMA Mkoa George Tito, amesema kwa sasa wanashughulikia suala la dhamana na kujua sababu za kukamatwa kwa Sugu pamoja na wanachama wengine ikiwa maandamano ni kitu cha kawaida kwani wananchi ni wapiga kura wake.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad