WAKATI vikao vya mchujo vikiendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kupata jina moja la mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwa madiwani, ubunge na uwakilishi, imebainika kuwa presha imepanda miongoni mwa wagombea wanaodaiwa kutumia rushwa kushinda katika mchakato huo wa kura za maoni.
Mchakato huo ambao ulianza Julai 20 mwaka huu kwa kuwachuja wagombea ubunge kupitia sanduku
la kura za maoni, ulikuwa na sura ya kipekee baada ya wagombea zaidi ya 10,000 kujitokeza katika kinyang’anyiro hicho.
CCM: TUTAWASHIKISHA ADABU
Aidha, akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humprey Polepole alisema chama hicho kitawashikisha adabu walioshinda kura za maoni kwa kukiuka maadili na makatazo ya chama.
Alisema wakati sasa vikao vya uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi vikiendelea kwa wagombea, wamepokea lundo la malalamiko katika ofi si yao.
Alisema kwa wagombea waliofuata sheria waendelee kuwa watulivu na kwa wale waliokiuka maadili katika chaguzi za kura za maoni, watawafundisha adabu.
“Wagombea waliofuata maadili watulie, mambo yanaendelea lakini kwa wale wenzetu waliokiuka maadili, mwaka huu mtajionea ‘surprise’ tutawashikisha adabu.
“Wachache waliojaribu kutoa rushwa, tutawashangaza kwa sababu mwaka 2016 mkutano mkuu wa chama, ulifanya mageuzi makubwa kuhakikisha vitendo hivi vinakoma,” alisema.
Kauli hiyo ya Polepole, ililandana na kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akihutubia Baraza la Idd al Haji, na kubainisha kuwa, wajumbe katika kura za maoni, wametoa mwongozo, lakini uamuzi uko katika vikao vya juu.
Alisema huo ni uthibitisho kwamba, vikao hivyo vinaweza kuja na matokeo tofauti na kura za maoni, hivyo walioongoza wakaenguliwa na waliodhaniwa wameshindwa wakaibuka washindi.
Waziri Mkuu alimtania aliyegombea ubunge jimbo la Handeni Vijijini, Hussein Msopa (Shehe Sharif Majini) akisema, “Mchakato unaendelea, tunakuombea sana basi kile kikao cha mwisho kikurudishe.
“Lakini waliokupa kura hizo ni wajumbe… wametoa mwongozo tu. Maamuzi yako juu huko tunaamini, Inshaallah kule Handeni utakuwa mbunge. Tunakuombea,” alisema.
Kwa mujibu wa Polepole, Kamati ya Siasa ya Wilaya kulingana na ratiba imeshakamilisha kazi yake, imejadili majina na kuweka mapendekezo kwa majina matatu na kueleza sababu za kupendekeza mojawapo.
Kamati ya Siasa ya Mkoa, pia nayo ilielezwa kukamilisha kazi yake Agosti 5 mwaka huu baada ya kujadili na kutoa mapendekezo.
Baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa, majina ya wagombea hao yanapelekwa kwa viongozi watendaji wa taifa kwa maana ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo kwa mujibu wa Polepole, watapitia taarifa nyingi zaidi ambazo ni za kiusalama na maadili.
“Baada ya hapo, tutakwenda kwenye Kamati Kuu, itajadili halafu baada ya hapo, itapeleka kwenye Halmashauri Kuu na mwenyekiti ni Ndugu Magufuli (Rais John), watapiga kura kuchagua jina moja ambalo mtu huyo atakuwa ndiye mgombea wa chama chetu cha mapinduzi katika kugombea ubunge katika majimbo,” alisema Polepole.
WALIOCHEZA RAFU ROHO JUU
Kauli za viongozi hao wa chama, zinakuja huku kukiwa rundo la malalamiko kwamba, katika baadhi ya maeneo, kura za maoni zilitawaliwa na vitendo vya rushwa huku baadhi ya wagombea wakinyooshewa vidole kwa rafu mbalimbali.
Miongoni mwa waliolalamika ni baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, waliotuhumu kuwapo vitendo vya rushwa kwenye kura za maoni.
Msimamizi wa Uchaguzi huo, Lazaro Manila alipozungumza na waandishi wa habari alisema “Tunatarajia kupokea taarifa mbalimbali zikiwamo pia za vyombo vya dola na kama kuna malalamiko kutoka kwa wapiga kura au wagombea, utaratibu unataka wayawasilishe kwa mamlaka zinazohusika yafanyiwe kazi.”
Vilevile Takukuru mkoani Arusha, ilikiri kuwakamata wagombea 20 wa nafasi ya ubunge katika jimbo la Arusha mjini, mshindi wa pili, Philemon Molel huku mshindi wa kwanza Mrisho Gambo, naye akichunguzwa.
Hata hivyo, vitendo hivyo viliendelea kulalamikiwa na baadhi ya wagombea wengine katika jimbo hilo ambalo sasa linazidisha presha kwa washindi hao.
Kwa upande wa Mbeya, nako aliyekuwa mgombea ubunge wa viti maalumu CCM, Dk. Marry Mwanjelwa, naye amekumbwa na tuhuma za rushwa baada ya clip ya video kuzunguka mitandaoni, huku ikidaiwa kumuonesha naibu waziri huyo na wajumbe wakipeana hongo.