Rais wa Tanzania ambaye pia ni mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) atachukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi hiyo wiki hii jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kuwa siku ya kiongozi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kuchukua fomu hiyo itatangazwa.
“NEC imetutangazia kuanzia leo tunaweza kuchukua fomu kwa ajili ya wagombea wa nafasi ya urais. Mwenyekiti wetu na Rais wetu ambaye pia ni mgombea urais kupitia chama chetu, Dkt. John Magufuli atachukua fomu wiki hii NEC, Dodoma akiomba dhamana ili akafanye makubwa zaidi kwenye muhula wa pili. Nitawaambia ni siku gani atachukua.
“Kampeni tutakazozifanya mwaka huu zitakuwa ni bora zaidi na zitakuwa za kisayansi. Kwa mujibu wa tafiti tuliyoifanya mwezi Juni mwaka huu, tunaingia kwenye uchaguzi tukiwa na mtaji wa wapiga kura milioni 16.8, ambao ni wanachama wa CCM, wapo wengine waliohamia hivi karibuni kabla ya Bunge kuvunjwa kama akina Silinde.
“Agosti 15, 2020 pale Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuna jambo, tutakuwa na tamasha kubwa la ndani la kutambulisha nyimbo za CCM za kabla ya kampeni, wakati wa kampeni na baada ya kampeni (kusherehekea ushindi), kutakuwa na wasanii (mmoja mmoja) 109 na bendi wakiwemo Diamond, Alikiba, Harmnonize, Billnas, Dudu Baya, Pam D, Mesen Selekta, Dulla Makabila, Haitham Kim, Shilole, Snura, n.k. Wataanza saa 4 asubuhi mpaka kesho saa 4,” amesema Polepole.