Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Emmanuel kipole kusimamia shughuli zote za mazishi katika msiba uliotokea wilayani humo baada ya nyumba kuungua moto iliyouwa watu sita usiku wa kuamkia ijumaa ya Agosti 21.
Mongella ametoa agizo hilo leo Agosti 22, 2020, alipofika msibani hapo kutoa pole kwa familia na kuwataka kujifunza kutokana na msiba huo na pia kumuombea majeruhi mmoja ambaye bado anaendelea na matibabu ili aweze kupona haraka.
‘’Kufiwa na ndugu wa familia moja tena kwa mpigo si jambo rahisi sana, majeruhi mmoja aliyepo hospitali tunamuombea kwa mungu aweze kupona haraka, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na timu yako msimamie hilo ili kwa upande wa serikali mtuwakilishe na muhakikishe hayo mazishi yafanyike kwa heshima kama inavyostahili’’, amesema Mongella.
Naye kamanda wa zimamoto mkoani Mwanza Ambwene Mwakibete amesema uchunguzi bado unaendelea na taarifa za awali zinaonesha kuwa huenda moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme.