SIRI imefichuka! Unaweza kusema hivyo, hiyo ni baada ya Simba kumsajili mchezaji Larry Bwalya, raia wa Zambia, ambaye inasemekana kuwa alikuwa ameingia makubaliano na Yanga.
Simba imefanikiwa kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 akitokea katika Klabu ya Power Dyamos ya nchini Zambia kwa mkataba wa miaka miwili.
Chanzo chetu cha kuaminika ndani ya Yanga kililiambia Championi Jumatatu kuwa, mchezaji huyo walishaingia naye makubaliano lakini akarubuniwa na wakala wake ambaye pia ni wakala wa Clatous Chama.
“Yanga tulikuwa tushaongea na Larry Bwalya lakini shida imetokea kwa kuwa wakala wake ndiye wakala aliyemleta Chama Simba hivyo ndio maana utaona dili liliharibika.
“Lakini pia imekuwa rahisi kwa Bwalya kujiunga na Simba kwa sababu kocha wa Simba, Sven (Vandenbroeck) ndiye kocha wa kwanza kumuita mchezaji huyo katika timu ya Taifa ya Zambia.
“Pia Clatous Chama ni mmoja wa wachezaji waliochangia Bwalya kwenda Simba kwa kuwa ni marafiki wa karibu na ukiangalia wote wanatoka katika taifa moja la Zambia huku wote wakiitumikia timu ya taifa,” kilisema chanzo hicho.
Naye Kaimu katibu Mkuu wa Yanga, Simon Patrick, alipotafutwa kuzungumzia juu ya suala hilo, alisema kuwa wao kama Yanga wamekuwa wakihusishwa na usajili wa wachezaji wengi lakini kuhusu usajili wao hakuna ambaye anafahamu.
“Tumekuwa tukihusishwa na usajili wa wachezaji wengi sana, lakini juu ya usajili wa wachezaji wetu, hasa wale wa nje, tumepanga iwe sapraizi kwa mashabiki wetu, hivyo watawafahamu wachezaji wapya wa nje hivi karibuni kwa kuwa muda wa kuja nchini ulishafika,” alisema kiongozi huyo.