SA’ Itakuwaje? Wimbo wa Harmo kwa Mkapa Kufutwa, Giza Nene, Rosa Ree Hausika


DAR: “Ikiwa Amen amen nenda salama kipenzi…
Amen amen tutazidi kukuenzi…
Tunakushukuru kwa yote mazuri uliyotufanyia…
Safari ni yetu sote leo mwenzetu umetangulia…
Nenda…nenda salama tutaonana kesho kiama…”

Hii ni sehemu ya mashairi yenye hisia kali za simanzi kutoka kwenye wimbo mpya wa staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’.



Wimbo huo unakwenda kwa jina la Amen alioachia Julai 25, mwaka huu kwenye Mtandao wa YouTube kisha ukatoweka ghafl a na kuwaacha Watanzania kwenye sintofahamu.



Wimbo huo maalum wa kuomboleza kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa mara baada ya kuachiwa, ulipokelewa vizuri kiasi cha kufanya vizuri na kushika nafasi ya pili kwenye trending za YouTube.



Kwenye wimbo huo Harmonize au Harmo amezungumzia uongozi wa Mkapa na utendaji kazi wake na mazuri yote aliyoyafanya kwenye nchi hii kipindi chote cha uongozi wake.



Wadau mbalimbali waliotoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii walionekana kupigwa na butwaa na kuhoji; ‘sa’ itakuwaje wimbo mzuri na unaomhusu kiongozi huyo muhimu ufutwe ghafl a na bila kujua sababu?

“Sa’ itakuwaje jamani wimbo pendwa wa maombolezo kama huu unafutwa wakati sisi bado tupo kwenye maombolezo, kwa nini ufutwe? Tatizo ni nini?” Alihoji jamaa anayejiita Kizdi mtandaoni.



NI HUJUMA?

Wengine walikwenda mbali zaidi kwa kuhoji kwa nini majanga kama haya yanamtokea Harmo mara kwa mara na si mwanamuziki mwingine.



“Watakuwa wanamfanyia hujuma tu jamani huyu Harmo wetu, kwa nini kila siku yeye tu? Watuachie huu wimbo wetu,” alisema mfuasi mwingine anayejiita Sherry.



KILICHOTOKEA…

Gazeti la IJUMAA linafahamu, kwenye wimbo huo mpya, umefutwa baada ya msanii wa muziki wa Hip Hop Bongo, Rosery Robert ‘Rosa Ree’ kuripoti kwenye Mtandao wa YouTube kwamba ameibiwa biti ya wimbo wake wa Kanyor Aleng aliouachia wiki mbili zilizopita.



Baada ya Rosa Ree kuripoti kwenye YouTube kumekuwa na tarifa ambayo inatolewa inayosomeka; “Video hii haipo kutokana na sababu za kihakimiliki kulingana na kile alichoripoti Rosa Ree.”



MAMENEJA WANENA

Akizungumza na gazeti hili juu ya ishu hizo, meneja wa Harmo, Beauty Mmary ‘Mjerumani’, alisema suala la wimbo wa Amen hawezi kulizungumzia kwa sasa kwa kuwa bado linafanyiwa kazi kiuongozi. “Bado tunalifuatilia, siwezi kusema chochote kwa sasa,” alisema Mjerumani.



Alipoulizwa analichukuliaje suala hilo kwani si mara ya kwanza linamtokea msanii wake, Mjerumani alisema ni mambo ya kawaida ambayo hutokea kwenye muziki ukizingatia kwamba vionjo vingi vya nyimbo za Kiafrika zinafanana.



“Harmonize siyo mwanamuziki wa kwanza kufutiwa nyimbo nchini na hata duniani, ni mambo ya kawaida sana kwenye muziki, ukizingatia hakuna vionjo vya muziki wa Afrika ambavyo mtu anakuwa navyo peke yake kwani ni aina ya muziki ambao hufanana kwa kiasi kikubwa.



“Ninawaomba mashabiki wa Harmonize watulie wakati suala hili linaendelea kufanyiwa kazi na tuna imani wimbo huo utarudi hewani,” alisema Mjerumani.



MENEJA MWINGINE…

Kwa upande wa meneja mwingine wa Harmo, Rajab Mchopa, alipotafutwa kuzungumzia ishu hiyo alijibu kuwa yuko msibani na hawezi kuzungumza kuhusiana na ishu hiyo. “Kwa sasa niko msibani, siwezi kuzungumzia ishu hiyo,’’ alisema Mchopa.



TUJIKUMBUSHE

Hii siyo mara ya kwanza kwa Harmo kufutiwa wimbo kwenye Mtandao wa YouTube, kwani Novemba, 2019 aliibua gumzo baada ya wimbo wake wa Uno alioutoa kwa mara ya kwanza tangu aachane na Lebo ya WCB kufutwa kwenye YouTube.



Hii ni baada ya mtayarishaji wa sauti ya wimbo huo, Magix Enga kutoka nchini Kenya kumpa wiki moja bosi huyo wa Lebo ya Konde Gang Music Worldwide kuuondoa wimbo huo kabla hajachukua hatua zaidi kutokana na kuchukua biti yake bila idhini yake.



Hata hivyo, baadaye waliyamaliza na wimbo huo kurejeshwa. Kama hiyo haitoshi, mwezi Machi, mwaka huu, Albam ya Harmo ya Afro Eeat ilifutwa kwenye baadhi ya mitandao baada ya kuelezwa kutokuwa na hakimiliki kwa baadhi ya vionjo vya nyimbo zake.



Kati ya waliomlalamikia Harmo anayefanya vizuri kwa sasa na Wimbo wa Fall in Love ni wale wasanii wa Morogoro wanaojiita Nego kupitia wimbo wao wa Kibanio ambao walidai kuwa Harmo aliwaibia biti na kuiweka kwenye wimbo wake wa I Miss You unaopatikana kwenye albam yake ya Afro East.

Stori: Happyness Masunga na Khadija Bakari, Ijumaa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad