KIKAO cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti, Elias Mwanjala, kimemalizika jioni hii ya leo.
Agosti 10 kulikuwa na kesi ya kuskilizwa kuhusiana na suala la kiungo mchezaji wa Yanga ambaye yupo kwenye mvutano na uongozi wa timu yake kwenye suala la mkataba.
Kuanzia asubuhi ya leo mpaka jioni kikao kilikuwa kikiendelea lakini hakuna maamuzi yoyote rasmi yaliyotangazwa kwa Waandishi wa Habari waliokuwepo viunga vya TFF, Karume, Jijini Dar Es Salaam.
Wadau wengi wa masuala ya michezo walijitokeza makao makuu ya TFF hali iliyopelekea Polisi kuingilia kati kuweka ulinzi na usalama kwa raia.
Mvutano mkubwa upo kwenye mkataba ambapo mchezaji anasema kuwa alisaini kandarasi ya miezi sita huku Yanga wakieleza kuwa alisaini kandarasi ya miaka miwili.
Agosti 8, saa nane, Simba ilimtambulisha mchezaji huyo kuwa mali ya Simba jambo ambalo liliamsha hisia kwa Yanga ambao walitoa taarifa kwamba wanalifuatilia suala hilo kwa ukaribu.