WADHAMINI wa Yanga, Kampuni ya GSM, imempa ofa kiungo mchezeshaji fundi wa Simba raia wa Sudan, Sharraf Eldin Shiboub kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo kwenye msimu ujao.
Kiungo huyo hivi sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kujiunga na klabu nyingine itakayomuhitaji katika msimu ujao kutokana na mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika ndani ya Simba huku dalili za kuongezewa zikiyeyuka.
Nyota huyo alitua Simba mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Al Hilal ya Sudan ambapo inaelezwa alisaini kwa dau la Sh Mil 100.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, juzi Yanga ilimpelekea Shiboub ofa hiyo, , lakini wakashindwana katika dau la usajili ambalo amewatajia mabosi hao ambalo ni siri.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo mwenyewe amekubali kujiunga na Yanga kama watakuwa tayari kutoa dau zuri la usajili ambalo yeye amelitaka na mshahara mnono.Aliongeza kuwa kiungo huyo juzi alirejea nyumbani kwao Sudan huku akiwaacha mabosi wa Yanga wajadiliane na kama wakifikia makubaliano mazuri, basi wamfuate wakiwa na dau ambalo yeye analitaka ili asaini.
“Yanga imeshindwana kidogo na Shiboub katika dau la usajili na kama wangempa lile ambalo analitaka yeye, basi angeshasaini mkataba tangu juzi kabla ya kurejea kwao Sudan.
“Shiboub ametaka dau kubwa ambalo mabosi wa Yanga ambao ni GSM wamelishindwa, lakini bado mazungumzo yanaendelea kati ya mchezaji na Yanga.“Ametoa sharti la kumfuata nyumbani kama Yanga watakuwa na kiasi hicho cha fedha ambacho amekitaka ili asaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mkurugenzi Uwekezaji wa Yanga, Injinia Hersi Said, juzi alisikika akisema: “Tunaendelea na usajili wetu wa siri wa wachezaji wazawa na kimataifa na mara baada ya kukamilika, basi haraka tutamtangaza mchezaji tuliyefikia naye muafaka mzuri na kusaini mkataba.”