KLABU ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck leo Agosti 22, imeibuka na ushindi wa mabao 6-0 mbele ya Vital’O ya Burundi kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Mchezo wa leo ulikuwa na lengo la kutambulisha wachezaji wapya pamoja na jezi itakayotumika kwa msimu wa 2020/21.
Ushindani ulikuwa mkubwa kipindi cha kwanza ambapo iliwabidi Simba wasubiri mpaka dakika ya 43 kupata bao la kwanza kupitia kwa Bernard Morrison ambaye alimaliza kazi ya pasi ndefu ya Larry Bwalya ambaye naye ni nyota mpya wa Simba.
Dakika mbili mbele, Morrison alitengeneza pasi kwa nahodha wa Simba John Bocco ambaye alipachika bao la pili dakika ya 45.
Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0 huku Vital’O ikiwa haijaambulia bao ndani ya dakika 45.
Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kwa wachezaji wake wote ambao walianza kikosi cha kwanza ambao ni Aishi Manula, Shomari Kapombe,Gadiel Michael,Ibrahim Ame,Joash Onyango,Jonas Mkude,Hassan Dilunga,Rarry Bwalya,John Bocco,Said Ndemla na Morrison.
Nyota walioingia ilikuwa ni pamoja na Beno Kakolanya ambaye aliumia dakika ya 64 na kumpisha Ally Salim, Mohamed Hussein,Keneddy Juma,Erasto Nyoni,Gerson Fraga,Mzamiru Yassin,Ibrahim Ajibu,Clatous Chama,Cris Mugalu, Charlse Ilanfya na Mirsaj Athuman.
Kikosi cha pili kilipachika mabao manne ambapo bao la tatu lilipachikwa na Chama dakika ya 56 akimalizia pasi ndefu ya Ajibu ambaye alifunga bao la nne dakika ya 75 kwa pasi ya Chama kisha bao la tano likapachikwa na Mugalu dakika ya 77 kwa pasi ya Miraj huku msumari wa mwisho ukipachikwa na Ilanfya kwa pasi ya Mohamed Hussein.
Sven amesema kuwa ulikuwa ni mchezo mgumu na mzuri huku wachezaji wake wakionyesha kile ambacho amewafundisha jambo ambalo linampa picha ya kikosi chake kuanza kufanya vizuri ndani ya ligi na mashindano mengine.