HATIMAYE siri imefichuka! Hivi ndivyo unavyoweza kusema, baada ya sababu zilizomwondoa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC, Senzo Mazingisa, ambaye jana alitangaza kujiuzulu nafasi yake ndani ya klabu hiyo na kujiunga na Timu ya Wananchi, Yanga SC.
Mhariri Mwandamizi wa Gazeti la Championi na mchambuzi mahiri wa masuala ya soka nchini, Saleh Ally Jembe, akizungumza katika kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio amesema kuwa moja ya sababu kuu zilizomwondoa Senzo katika Klabu ya Simba ni kwamba alishindwana na Simba kuhusu malipo ya mkataba wake mpya, kwani kiasi alichoomba kuongezewa, Simba waligoma kutoa.
“Yanga SC kumpata Senzo ni faida, kutokana na walivyokuwa wanajiendesha walitakiwa kupata mtu kama huyu, lakini najiuliza watamuingizaje kwenye mfumo wao, sababu kwa katiba ya Yanga hawana CEO, labda wampe Senzo ukatibu mkuu ili aweze kufanya majukumu yake.
“Ukisema Senzo kachukuliwa Simba SC ni makosa, sababu yeye na Simba walikuwa wameshashindwana, alikuwa huru kuondoka, aliomba kwenye mkataba mpya aongezewe mzigo, Simba wakasema mzigo huu hatuwezi kulipa. akasema mimi nitaondoka, Yanga wakapata taarifa wakamwahi.
“Jana niliongea na Engineer. Hersi nikamwambia katika move zote ulizofanya kuelekea msimu ujao hii ya Senzo ni sahihi zaidi, sababu atakuwa mshauri mzuri, ni mzoefu, ana nafasi ya kumwambia hapa tumepatia hapa tumekosea, tunahitaji kocha wa namna gani, forward wa namna gani.