Skendo Zilivyokwanyua Utajiri wa Mastaa Hawa



BADO Kenya inaendelea kujisafisha kwenye suala la skendo za matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwa wanariadha wake.
Sheria za mchezo wa riadha zimekuwa ngumu wakati huu kwani wanariadha wakorofi waliokuwa na mazoea ya kukwepa vipimo siku hizi imekula kwao. Hawana ujanja.
Tofauti na zamani siku hizi wanafanyiwa vipimo vya mara kwa mara tena kwa kushtukizwa. Zamani walikuwa wanapewa tarahe ambazo sampo zao za kupimwa zilichukuliwa, hivyo wakawa wanajua wakati gani wa kutumia dawa hizo na muda wa kuacha ili kusafisha damu kabla ya wakaguzi kuwafikia.
Tangu kanuni zibadilike, wanariadha wengi wa Kenya wamejikuta matatani. Wengi wameishia kujiunga na orodha nzito ya wanamichezo wengine wa majuu waliopoteza dili kubwa za matangazo baada ya kukumbwa na skendo mbalimbali ikiwemo matumizi ya dawa hizo. Hawa ni mifano ya wanamichezo hao.


RITA JEPTOO
Skendo: Dawa
Hasara: Dola 625,000
Baada Mkenya huyu kufeli katika vipimo 2016, staa huyu wa marathon alipigwa marufuku miaka minne kushiriki riadha. Vilevile alipokonywa ubingwa wake wa Boston Marathon 2014 na pia kuamrishwa arejeshe kitita cha dola 150,000 (zaidi ya Sh300 milioni) alizolipwa kwa ushindi huo pamoja na nyongeza nyingine ya dola 25,000 (zaidi ya Sh50 milioni) zilizokuwa bonasi.
Haikuishia hapo, Jeptoo alipoteza michongo zaidi ikiwemo kitita kizito cha dola 500,000 (zaidi ya Sh1 bilioni). Fedha hizo alipaswa kulipwa kwa kuibuka bingwa wa mbio za marathoni za dunia (World Major Marathon - WMM) mwaka 2013-14, lakini skendo hiyo ikambadilishia mambo.


JEMIMA SUMGONG
Skendo: Dawa
Hasara: Dola 390,000
Januari mwaka huu, marufuku ya awali ya kufungiwa kushiriki riadha kwa miaka minne iliongezwa nyingine na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) hadi miaka minane. Hii ina maana kuwa Sumsong (34) anaweza kurejea katika riadha akiwa na miaka 42. Kwa ufupi riadha kwake ni kama imekwisha. Bingwa huyo wa marathoni aliyeweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwashindia Wakenya medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki kule Rio De Janeiro 2016, aliingia hasara kubwa. Ndoto yake ya kutetea ubingwa wake wa London Marathon 2017 ilizimwa ambapo alikuwa na uhakika wa kuibuka mshindi kutokana na ushindani hafifu uliokuwepo kipindi hicho.


MAGIC JOHNSON
Skendo: Ukimwi
Hasara: Dola 25 milioni
Bingwa huyu mara tano wa mchezo wa kikapu katika Ligi ya NBA, Marekani alipoteza zaidi ya Sh2.5 bilioni alipotangaza 1991 kwamba anastaafu baada ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi. Kampuni nyingi kubwa ikiwemo Pepsi na Converse zilisitisha mikataba ya biashara na matangazo waliyokubaliana.


BEN JOHNSON
Skendo: Dawa
Hasara: Dola 2.8 millioni
Ni bingwa wa zamani wa dunia kwenye mbio fupi za mita 100. Aliweka rekodi ya dunia kwenye Olimpiki za 1998. Hata hivyo, baada ya siku tatu alipokonywa ushindi huo damu na mkojo wake ulipopatikana na chembechembe za dawa zilizopigwa marufuku za stanozolol aina ya steroid zinazodaiwa husisimua misuli na kumwongeza mtu nguvu. Kampuni ya Kiitaliano ya Diadora mara moja ilisitisha mkataba wa matangazo ambao ungemlipa zaidi ya Sh5.5 bilioni



OSCAR PISTORIUS
Skendo: Mauaji
Hasara: Dola 2 milioni
Advertisement
Kipaji cha mwanariadha huyu wa Afrika Kusini asiye na miguu, kilikwama 2013 baada ya kupatikana na kosa la mauji ya mpenzi wake Reeva Steenkamp. Kesi hiyo ilimsababishia kupoteza dili kibao za maana na kampuni mbalimbali ikiwemo Nike na Oakley ambazo kwa pamoja zilikuwa zikimlipa zaidi ya Sh4 bilioni kila mwaka.


MARIA SHARAPOVA
Skendo: Dawa
Hasara: Dola 70 milioni
Kwenye utajiri wa wachezaji tenisi hasa wa kike, wengi wanamfahamu Serena Williams, ila kipato chake hakimfikii Maria Sharapova.
Kampuni za Nike, Porsche na Tag Heuer zote ziliachana naye kwenye dili zao za matangazo baada ya kuthibitika kutumia dawa zilizopigwa marufuku mwaka 2016.
Kampuni ya Nike ndio iliyokuwa ikimpa mchongo wa maana baada ya kufuta mkataba wa miaka minane uliokadiriwa kuwa na thamani ya dola 70 milioni (zaidi ya Sh14 bilioni).


MANNY PACQUIAO
Skendo: Kupinga ushoga
Hasara: Dola 10 milioni
Manny Pacquiao ni kati ya maboksa wenye utajiri mkubwa duniani akiwa na mkwanja unaokadiriwa kufikia dola 200 milioni (zaidi ya Sh400 bilioni). Hata hivyo, mwaka 2016 alijikuta akikimbiwa na baadhi ya kampuni alizoingia nazo mikataba ya matangazo baada ya kutoa kauli za kupinga ushoga.
Licha ya kuomba radhi baada ya kauli hiyo ‘kutrendi’ sana, Nike walimpiga chini na kumsababishia kupoteza dili ya miaka mingi iliyokadiriwa kuwa zaidi za dola 10 milioni (zaidi ya Sh20 bilioni).


MIKE TYSON
Skendo: Ugomvi nyumbani
Hasara: Dola 10 millioni
Tyson ni bondia mkali ambaye mpaka sasa jina lake limesalia kwenye ulingo wa ndondi. Hata hivyo, alikumbwa na kashfa kibao zilizochangia kumpunguzia kipato.
Kampuni ya Pepsi ilimpiga chini 1998 kwenye dili zao za kumtumia kama balozi wa matangazo wa bidhaa zake, baada ya aliyekuwa mkewe kumkashifu kwa kumnyanyasa mara kwa mara nyumbani ikiwamo kumpiga.


TIGER WOODS
Skendo: Mchepuko
Hasara: Dola 20 milioni
Miaka ya nyuma aliwika sana akitajwa kuwa mchezaji bora wa gofu duniani. Hata hivyo, kando na mafanikio hayo kumpa heshima na kumzidishia umaarufu, pia yalimzidishia mkwanja kupitia mikataba ya matangazo na kampuni kibao.
Lakini nyota yake ilianza kufifia mwaka 2013 alipokiri kuchepuka dhidi ya mkewe.
Baada ya kashfa hiyo kuibuka kampuni kibao zilijiondoa kwenye mikataba naye zikiwemo Gillette, Accenture, AT&T, Gatorade na Tag Heuer ambazo kwa pamoja zilichangia kumwingizia hasara ya zaidi ya dola 20 milioni (zaidi ya Sh40 bilioni).
Kwa sasa Woods ameanza kurejea taratibu katika mchezo wa gofu, lakini hata hivyo jina lake limeshindwa kung’ara na kusikika masikioni mwa watu kama ilivyokuwa kabla ya kukumbwa na kashfa ya ngono.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad