Tanzania Ni Ya Kwanza Afrika Kwa Kusambaza Umeme Hadi Vijijini - Waziri Mkuu



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania imeshika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kufanikiwa kusambaza umeme nchini kote kwa asilimia 80.

“Leo hii Tanzania ni ya kwanza barani Afrika kwa kusambaza umeme kote nchini hadi vijijini na kufikisha asilimia 80. Kuna nchi ngapi barani Afrika, lakini Tanzania imefanikiwa kuwa ya kwanza. Tumeweza kufikia vijiji 9,112 Tanzania na hadi Aprili 2020 na tumetumia shilingi trilioni 2.27,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatatu, Agosti 17, 2020) wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye mkutano wa viongozi wa dini kutoka kamati za amani za mikoa mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar, uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na viongozi waliohudhuria mkutano huo uliandaliwa ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake katika ustawi wa amani, uzalendo na kumtanguliza Mungu, Waziri Mkuu amesema ushirikiano mkubwa wanauonesha kwa Serikali, umewezesha kufanya mambo mengi ikiwemo kuimarisha huduma za upatikanaji wa nishati kwa ajili ya ustawi wa Watanzania.

Mbali ya upatikanaji wa umeme nchini, Waziri Mkuu ameelezea mambo mengine 15 yaliyofanyika kwa ufanisi mkubwa chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli ikiwemo kurejesha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma; mapambano dhidi ya dawa za kulevya; ulinzi wa raslimali za Taifa; kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na kukua kwa uchumi.

Mengine ni mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa ajira; ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya afya; maboresho ya elimu; huduma za maji; ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Nyerere, ujenzi wa mradi wa reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR); usafiri wa anga; ujenzi wa meli na bandari na ujenzi wa barabara na madaraja.

Akielezea kuhusu kuondoa umaskini na ukosefu wa ajira, Waziri Mkuu amesema kupitia sekta kuu za viwanda, kilimo, biashara, madini, utalii, miundombinu ya kimkakati pamoja na mifumo ya mikopo nafuu, Serikali imezalisha ajira za kutosha kwa Watanzania.

“Kupitia ujenzi wa viwanda vipya, tumetengeneza jumla ya ajira zipatazo 482,601 na kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya SGR, Stieglers’ Gorge, ujenzi wa shule, hospitali na ufufuaji wa mashirika yetu tumefanikiwa kutengeneza ajira zipatazo 6,032,299.”

“Tunao uwezo wa kuhimili ujenzi wa viwanda vipya na nipende kuwahakikishia wenye mitaji kwamba Tanzania ni mahali salama pa kuwekeza. Tulianza na mazao matano ya kimkakati lakini sasa tumeyaongeza. Kupitia kilimo tunazalisha mazao ambayo ni malighafi kwa viwanda vyetu,” amesema.

“Suala la ajira ni kilio cha wote lakini kila nchi inatumia njia yake kukabliana nayo. Je tusingekuwa na miradi ya kimkakati kama SGR na Stieglers’ Gorge, hawa watu milioni sita na zaidi wangekuwa wapi kwa sasa?”

Mapema, akitoa wasilisho la viongozi wa dini, Katibu wa Kamati ya Amani, Askofu Jackson Sosthenes alisema lengo la mkutano wao ni kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua iliyofikiwa ambayo Tanzania imefikia kabla ya mwaka 2025, kina miatno kabla ya muda uliopangwa.

“Viongozi wa Serikali ya awamu ya tano wameweza kufikia matarajio ya wengi na wamekuwa siyo watu wa maneno mengi. Siri ya yote hayo ni kumtanguliza Mwenyezi Mungu kama ilivyosemwa kwwenye maandiko matakatifu kwamba mtafuteni kwanza Mungu na mengine yote mtazidishiwa,” amesema.

Akitoa tamko la viongozi wa dini, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Sheikh Alhad Mussa alisema ujasiri wa Rais Magufuli wa kutozuia ibada na kukata kufungia watu ndani (lockdown), ulimpendeza Mwenyezi Mungu na akaamua kuifanya Tanzania kuwa nyota inayong’ara ulimwenguni.

Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, Sheikh Alhad alisema: “Viongozi wa dini hatuko tayari kushuhudia uvunjifu wa amani ukitendeka nchini. Tunawaomba viongozi wa saisa wahakikishe wanalinda amani yetu na mshikamano wetu.”

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeiry ambaye alikuwa wa kwanza kutoa salamu za viongozi wakuu wa dini, alisema mtu mwenye akili anahitaji pointi ndogo tu kuona kinachofanywa na Rais Magufuli.

“Mambo aliyoyafanya Mheshimiwa Rais kwa nchi yetu hayahitaji kufikiri sana kwa sababu yako dhahiri. Amefanya kazi kubwa ndani ya miaka mitano, ambayo yangeweza kufanyika kwa miaka 25.”

Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa alisema amani ndiyo msingi wa maendeleo yote. “Amani ni mtaji wa maendeleo. Ukiwa na fedha lakini kama hakuna amani, haziwezi kukusaidia chochote.”

“Viashiria vya ukosefu wa amani hatuvipendi, na tunaviombea vitoweke katika jina la Mungu,” alisema na kuongeza kuwa viongozi wa siasa watambue kuwa yako maisha wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

“Sisi viongozi wa dini tutaendelea kuiombea nchi yetu. Mungu anaipenda sana Tanzania, na hata tulipopita kwenye bonde la uvuli wa mauti la COVID 19, bado alituvusha. Tuendelee kumheshimu Mungu, kumtii na tuendelee kumwabudu Mungu,” alisisitiza.

Akizungumza kwa niaba ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Nooman Jongo alisema zamani Tanzania iliathiriwa sana mambo matatu ya udini, ukabila na uchama lakini kwa sasa hayapo. “Ukiwa Mkristo au Muislamu unapaswa utambue kuwa sisi sote ni ndugu wa baba mmoja, ambaye ni Ibrahimu. Tuangalie amani na upendo na yaliyofanywa na Rais John Pombe Magufuli hayahitaji tochi ili uyaone,” alisema.

Naye Askofu Michael Hafidhi wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar aliwataka viongozi wa vyama vya siasa waache kuwasema wenzao vibaya na kutumia majina ya maaskofu na sheikh kwa manufaa yao binafsi.

“Zamani tulikuwa na siasa chafu, siasa za majitaka. Je sasa hivi zinatoka wapi? Tafadhali tusirudi tena kule nyuma. Wako baadhi ya viongozi wa siasa, wakipanda majukwani wanawasema wenzao, waache mara moja.”

“Tena kuna wanatumia majina ya Masheikh na Maaskofu vibaya. Msitufanyie reference katika majukwaa yenu kwa sababu sisi tunafanyiwa reference na Mwenyezi Mungu. Wakiendele kututumia, wajue tunahesabu zao siku,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Mchg. George Fupe alisema wanatoa tamko kwa wagombea wote watakaoenda kujinadi kwenye kampeni ili kutunza amani ya nchi ya Tanzania.

“Tamko letu kwa wagombea wote, lina mambo matatu: Tunawataka wamtangulize Mungu katika utendaji wao, pili watumie busara na hekima wawapo na tatu wazingatie utu wema.”

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad