Rais wa Marekani Donald Trump anataka yeye na mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wa dawa kabla ya mjadala wao wa kwanza mwezi ujao.
Bwana Trump aliambia gazeti la Washington Examiner kwamba amegundua maboresho ya ghafla katika utendaji wa Bw. Biden katika mijadala ya Televisheni ya chama cha Democratic.
Rais hakutoa ushahidi wa jinsi alivyofikia madai kwamba mpinzani wake huenda anatumia madawa kando na kusema : "Naelewa mambo haya."
Bw. Biden na Bw. Trump watashiriki mjadala wa umma mara tatu kabla ya uchaguzi mkuu wa urais utakaoandaliwa Novemba tarehe tatu.
Mwaka 2016, Bw. Trump aliashiria aliyekuwa mpinzani wake wa-Democratic, wakati huo Hillary Clinton, alikuwa "akipuliziwa madawa" kabla ya mijadala yao na kumtaka afanyiwe uchunguzi wa utumizi wa dawa za kulevya kabla ya kukutana tena katika mjadala wa moja kwa moja kwenye Televisheni. Kampeini ya Clinton ilipuuzilia mbali madai hayo.
Siku ya Jumatano, rais - ambaye anatarajiwa kuhutubia kongamano linaloendelea la chama cha Republican Alhamisi - alitoa madai kama hayo, akihoji kuimarika kwa uwezo wa Biden kujadili masuala hasa katika mjadala wake wa mwisho.
Bw. Trump alisema naibu huyo wa zamani wa rais wa Marekani "hakua na uwezo wa kujieleza vyema" katika baadhi ya mijadala 11 ya moja kwa moja kwenye Tevisheni alipokabiliana na kundi la wagombea msimu wa uchaguzi wa Democratic.
Walipofikia mjadala wa mwisho Machi 15, uwanja wa makabiliano ulikuwa umesalia na Bw. Biden na Seneta wa Vermont Bernie Sanders.
Bw. Trump aliambia Washington Examiner: "Sielewi jinsi [Bw. Biden] aliyekuwa akitetereka katika mijadala alivyoimarika ghafla na kumshinda Bernie."
Aliongeza: "Sio kwamba alimfikia Winston Churchill kwasababu hawezi, lakini ulikuwa mjadala wa kawaida tu.
"Hakuna kikubwa kilichojitokeza na ukweli ni kwamba tutaitisha uchunguzi wa dawa za kulevya kwasababu hakuna jinsi - anaweza kufanya hivyo bila kichocheo."
Mijadala mitatu ya urais itafanyika Cleveland, Ohio, Septemba 29; Miami, Florida, Oktoba 15; na Nashville, Tennessee, Oktoba 22.
Bw. Trump aliomba kufanya mijadala zaidi na Bw. Biden, lakini Tume inayosimamia Mijadala ya Urais ilipinga ombi hilo. Pia aliomba mjadala wa kwanza uandaliwe mapema kwa manufaa ya wapiga kura wa awali, lakini ombi hilo halikuridhiwa.
Bw. Trump, 74, na Bw.rBiden, 77, wamekuwa wakirushiana cheche za maneno kuhusu suala la kuwa na matatizo ya kiakili.