Serikali ya Ufaransa inatuma kikosi cha polisi wa kutuliza ghasia kwenda jimbo la Marseille (Marseye) kusaidia utekelezaji wa sharti la kuvaa barakoa kwa lengo la kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.
Msemaji wa serikali mjini Paris Gabriel Attal ametangaza leo kuwa maafisa 130 wa polisi wanapelekwa kwenye jimbo hilo ambalo Ijumaa iliyopita lilitanua amri yake ya uvaaji barokoa kwenye masoko na maeneo mengine.
Hatua hiyo ya kutuma polisi wa ziada inakuja wakati mji mkuu Paris na miji mingine nchini Ufaransa imetangaza masharti ya uvaaji barakoa katika maeneo ya wazi kuanzia leo Jumatatu.
Ufaransa imeshuhudia visa vya hapa na pale vya vurugu zinazofanywa na watu wanaopinga amri ya kuvaa barakoa katika taifa hilo lenye idadi ya vifo 30,400 vilivyotokana na janga la virusi vya corona.
Maambukizi ya COVID-19 yamepanda nchini Ufaransa, na hapo jana nchini hiyo ilirikodi visa vipya 3,015, ambayo ni idadi kubwa kabisa tangu vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona vilipoondolewa mnamo mwezi Mei.