BAADA ya kutambulisha vifaa vyao vipya ambavyo watavitumia kwa msimu ujao akiwemo beki Bakari Mwamnyeto, mabosi wa Yanga, wiki ijayo wanatarajiwa kumshusha kocha mkuu wa timu hiyo ambaye atakuja kubeba mikoba ya Mbelgiji, Luc Eymael ambaye alitimuliwa.
Mabosi hao wamepanga kumshusha kocha huyo mapema baada ya kamati maalum ambayo ilipewa kazi ya kumtafuta kufikia mwishoni huku wakipanga kocha huyo atue mapema kwa ajili ya kuwahi kambi ya timu hiyo itakayoanza Agosti 10, mwaka huu.
Miongoni mwa majina ya makocha ambao waliomba nafasi ya kurithi nafasi hiyo ya Eymael ni makocha wa Tanzania, wanaotokea Afrika na kutoka barani Ulaya.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said ambao ni wadhamini wa Yanga, amesema kuwa watamleta kocha huyo kwa kuwa mchakato wa kumpata upo mwishoni, ambapo hadi wiki ijayo watakuwa tayari wameshamleta nchini kwa ajili ya kuanza majukumu yake ikiwemo ya kuleta muunganiko wa mastaa wao ambao wamewasajili hadi sasa.
Hersi ameongeza kwamba kuwa kocha huyo analetwa kwa ajili ya kuivusha klabu hiyo na kufikia mafanikio ambayo wanayataka kwa msimu ujao.“Suala la kocha tupo kwenye mchakato wa mwisho wa kumpata, kamati inaendelea kufanya kazi yake kupitia maombi hayo ambayo yanatoka kila sehemu ya dunia.
Wapo makocha wa Tanzania, Afrika na hata Ulaya.“Hadi wiki ijayo tutakuwa tumeshamtangaza kocha kwa ajili ya kuwahi kambi ambayo tutaanza Agosti 10.
Tunataka kumleta kocha wa kweli ambaye atatuvusha kwenda kwenye mafanikio.“Tunataka awahi mapema kwa sababu hakuna muda wa kupoteza na pia wachezaji wetu wanataka kuzoeana kwa mapema hivyo ni muhimu yeye akawepo mapema,” alimaliza Hersi