Usajili Mpya Simba Visu Viputu




BAADA ya majina kadhaa kutajwa kuwa mbioni kusajiliwa na Simba, klabu hiyo imewataka wapenzi wao kuendelea kutega masikio kwani muda si mrefu, vifaa vya nguvu zitaanza kushushwa Msimbazi.

Tangu mwezi uliopita, kumekuwapo kwa majina ya wachezaji kadha wa kadha wa kigeni na wazawa wanaotajwa kuwa katika mpango wa kusajiliwa na Simba.

Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa, yupo nyota wa Yanga, Bernard Morrison, lakini pia Papy Tshishimbi wa Wanajangwani hao.

Kati yao, Morrison ameonekana kuwateka zaidi wapenzi wa Simba, wakimkumbuka kutokana na bao lake alilowafunga walipokuatana Yanga Machi 8, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tayari watu wa Yanga wameanza kumsahahu Morrison kutokana na jinsi anavyowasumbua, zaidi wakikerwa na kitendo chake cha kutoka uwanjani alipofanyiwa mabadiliko walipovaana na Simba Julai 12, mwaka huu na kupokea kipigo cha mabao 4-21.

Juu ya Tshishimbi, naye anatajwa kuwa mbioni kutua Simba, hilo likichangiwa na kitendo chake cha kuwazungumsha Yanga katika suala zima la kuongeza mkataba mpya.

Ukiachana na hao, kuna jina la Michael Sarpong, mshambuliaji hatari anayekipiga Rayon Sports ya Rwanda ambaye naye anatajwa kuwa katika mipango ya Simba msimu ujao.

Akizungumzia juu ya usajili wao wa msimu ujao, Ofisa Mtendaji wa Simba, Senzo Mbatha, alisema: “Ninachoweza kusema ni kwamba tumejipanga kufanya usajili mkubwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi ya ndani na michuano ya Ligi ya Mabingwa.”

Alisema usajili wao lazima uwe wa kimataifa kwa kuchukua wachezaji wazuri watakaoweza kuisaidia timu yao katika ligi ya ndani na kimataifa na si kuokota ukota tu ilimradi ni mchezaji.

Senzo alisema licha ya kuwa na muda mchache kabla ya kuanza kwa msimu ujao, ikiwa ni pamoja na tamasha maalum la Siku ya Simba (Simba Day), lazima wafanye mabadiliko kwa kuongeza baadhi ya wachezaji wa kigeni, lakini wakiwa ni wenye uwezo wa hali ya juu.

“Kuna wachezaji lazima waondoke ili tuweze kujenda kikosi bora cha kimataifa, usajili huo utasaidia kwenye timu yetu kuwa moja ya timu bora Afrika,” alisema Senzo.

Aidha, Senzo alisema mara baada ya mchezo wao wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) dhidi ya Namungo, wataanza maandalizi ya Simba Day, tamasha ambalo hufanyika Agosti 8, mwaka ya kila mwaka.

Alisema baada ya hapo, wataanza kushusha vifaa vyao mmoja baada ya mwingine, hivyo wapenzi wao wakae mkao wa kula
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad