Usichokijua Kuhusu Watu Wanaocheza Na Majeneza


KATIKA jamii zetu hususan Tanzania, msiba umekuwa ukiombolezwa kwa huzuni zinazotawaliwa na vilio kutoka kwa wafiwa ambao ni ndugu na marafiki kwa ujumla kutokana na kuondokewa kwa mtu wao huyo muhimu.

Lakini kwa nchi nyingine Afrika kama Ghana, msiba umekuwa ukiendeshwa tofauti na utamaduni tuliouzoea. Wao hufanya msiba kama zilivyo sherehe nyingine za furaha. Huwaburudisha kwa kuwaondolea huzuni wafiwa kwa kucheza na kufurahi pamoja na kumsindikiza vizuri marehemu huyo kwenye makazi yake ya kudumu yaani kaburini.


Kama umekuwa ukifuatilia vizuri kwenye mitandao ya kijamii, basi utakuwa umeona video zikiwaonesha watu (vijana walioshiba) wakifanya mzaha kwa kucheza na jeneza linalosemekana kuwa na mwili wa marehemu ndani yake.

Je, unawajua ni akina nani na ni kwa nini wanafanya hivyo? Gazeti la IJUMAA limechimba ambapo linakuletea usichokijua kuhusu jamaa hao;

HISTORIA

The Kissing Brandit ni kikundi kinachoratibu shughuli za mazishi nchini Ghana. Kikundi hiki huwa na watu kuanzia wanne hadi sita msibani ambao huvalia sare za suti nyeusi na kucheza kwa staili moja ambayo hutoa vionjo mbalimbali vya kucheza na jeneza kwa lengo la kuwaburudisha wafiwa kuondokana na huzuni ya kumpoteza kipenzi chao.

Benjamin Aidoo ndiye mwanzilishi wa kikundi hicho. Tangu mwaka 2002, Aidoo alikuwa akifanya kazi kama mhudumu ya mochwari nchini humo. Lakini baadaye mwaka 2017 ndipo akapata wazo la kuanzisha kikundi hicho ili kuweza kujipatia kipato yeye pamoja na watu wengine.

Lakini kwa kipindi cha sasa, kikundi hiki kimekuwa maarufu zaidi ulimwenguni kutokana na watu kurusha video za watu wanaofanya mzaha kama kuendesha gari kwa spidi kisha wanatokea watu hao wanaocheza na majeneza kwa lengo la kumtisha mtu anayefanya mzaha unaoweza kumsababishia kifo.

UBUNIFU

Aidoo anahitaji kupata pongezi za hali ya juu, kwani ameweza kubuni kitu cha tofauti mno ambacho kinapendwa na wengi kwenye jamii.


Mbali na kubuni mavazi kama suti nyeusi, viatu, tai nyeupe au kitambaa cheupe, kofia, gloves pamoja na miwani, pia wamebuni staili mbalimbali za kucheza wakiwa wamelibeba jeneza; ambapo hucheza wakiwa wamesimama, wameinama, wakilala, kupiga magoti na hata kukaa chini au kugaragara mavumbini wakiwa na jeneza lenye mwili wa marehemu.

Licha ya kutoa mbwembwe hizo msibani, lakini pia huwauliza wafiwa kama wanahitaji wacheze au lah! Kama wasipotakiwa kucheza, hubeba jeneza tu na kuanza kutembea kwa stepu kuendana na biti yao ya muziki huku wakiwa ‘siriaz’. Lakini kama wameambiwa wacheze, basi hucheza kulingana na kiwango cha pesa watakacholipwa.

MAFANIKIO

Ingawa watu wataona kama ni kitu cha kushangaza hususan kwenye utamaduni wa jamii yetu, lakini ni fursa ya kujiingizia kipato. Kwa taarifa yako, kule nchini Ghana, watu wako radhi wakope pesa kwa lengo la kukodi kikundi hicho kiwaburudishe wanapokuwa kwenye majonzi.

Vilevile kikundi hiki kimeweza kutoa ajira kwa vijana zaidi ya mia moja, kutokana na kukubalika kwao kwenye jamii. Hii imewasaidia vijana hao kumudu maisha yao na kuwaepusha kujiingiza kwenye magenge ya uhalifu kama uporaji, ujambazi na kadhalika.

CHANGAMOTO

Hakuna kazi isiyokuwa na changamoto. Hata kikundi hiki nacho hupitia changamoto kadhaa. Aidoo anasema, wakati wakiwa kwenye mazishi huku wakicheza na jeneza, ghafla jeneza linaweza kudondoka na kupasuka, hivyo inawalazimu kuwa makini mno. Pia changamoto nyingine wanayokumbana nayo ni katika uchezaji, unakuta wakati mwingine mtu anasahau staili ya kucheza na kadhalika hivyo kujikuta wakipishana katika uchezaji.

Kibongobongo kuna vikundi vya kulia kwenye misiba, lakini vya staili hii ya kucheza na jeneza lenye mwili wa marehemu havipo! Unaonaje kikianzishwa kikundi cha aina hii hapa Bongo? Kitakuwa na mashiko? Fursa hiyo hapo, kazi ni kwako!

MAKALA | Makala: Amina Said

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad